Ufaransa yalaani ukandamizaji RD Congo

Muktasari:

“Ufaransa inarudia kuweka msisitizo juu ya wito wake wa kuheshimu haki za binadamu na misingi ya uhuru unaoanza na haki yao ya kupinga.”

Paris, Ufaransa. Ufaransa imevilaumu vikosi vya usalama vya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kwa kuua watu sita na kujeruhi wengine makumi katika maandamano ya kumpinga Rais Joseph Kabila yaliyoandaliwa na Kanisa Katoliki.

“Ufaransa inalaani vikali machafuko yaliyosababishwa na vikosi vya usalama wakati wa maandamano ya Januari 21, 2018,” ilisema taarifa ya msemaji wa wizara ya mambo ya nje.

“Ufaransa inarudia kuweka msisitizo juu ya wito wake wa kuheshimu haki za binadamu na misingi ya uhuru unaoanza na haki yao ya kupinga.”

Ufaransa imeonyesha wasiwasi wake kuhusu machafuko na vitisho dhidi ya waangalizi wa Umoja wa Mataifa na imetoa wito kwa mamlaka za RD Congo kufanya uchunguzi wa wazi juu ya vurugu hizo na waliosababisha wachukuliwe hatua za kisheria.

Hatua ya Kabila kukataa kung’atuka madarakani baada ya kipindi cha uongozi kumalizika Desemba 2016 kimechochea mfululizo wa maandamano mitaani ambayo watu kadhaa wameuawa Kinshasa. Hatua yake hiyo imehamasisha vikundi vya waasi katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Katika taarifa hiyo, Ufaransa imesema “iko tayari kusaidia mchakato wa uchaguzi wenye lengo la kuhakikisha unafanyika kwa uhuru na kubadilishana mamlaka kidemokrasia ndani ya RD Congo.”