Ufisadi, rushwa unavyotafuna miradi ya ujenzi

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki

Muktasari:

  • Fedha zinazopotea katika miradi ya ujenzi huchangia bei kupanda na miundombinu kujengwa kwa viwango vya chini.

Dar es Salaam. Takwimu za uchambuzi wa utekelezaji wa miradi zinaonyesha kati ya asilimia 10 hadi 30 ya fedha zinazotolewa katika miradi ya ujenzi hupotea kutokana na uzembe, ukosefu wa weledi, ufisadi na rushwa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki amesema hayo akifungua warsha ya uwazi wa taasisi za ununuzi iliyoandaliwa na mkakati wa uwazi na uwajibikaji katika ujenzi Tanzania (CoST).

Kairuki alisema jana Alhamisi kuwa, kiasi hicho cha fedha kinachopotea kinachangia bei ya miradi kupanda, miundombinu kujengwa kwa viwango vya chini na kuhatarisha usalama wa wananchi.

Kutokana na hilo, amezitaka taasisi za umma kuweka na kuimarisha mifumo ya uwazi na uwajibikaji ili kuendana na dhana ya utawala bora.

Amesema endapo taasisi hizo zitazingatia hilo itakuwa rahisi kuwaletea wananchi maendeleo kwa haraka kwa kuwa hakutakuwepo mazingira ya rushwa.

“Tumeshuhudia baadhi ya majengo yakiporomoka na barabara kuharibika muda mchache baada ya kuzinduliwa, jambo hili halitavumilika. Nawasihi wadau wote kuonyesha uzalendo na tuwajibike kuhakikisha fedha za umma zinaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo,” amesema.

Pia, amezitaka taasisi za ununuzi kutosita kutoa taarifa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru) endapo wataona kuna utata katika mchakato wa ununuzi kutokana na kukuikwa kwa utaratibu.

Amesema, “Kwa mwelekeo wa Serikali ni muhimu kuzingatia misingi ya sheria na utaratibu. Kama unaona kuna ukiukwaji wa utaratibu usisite kutoa taarifa, usiogope wala kuona haya kwa kuwa ikija kutokea tatizo utawajibika nalo.”

Kairuki amesema, “Kuondokana na hilo, kila kitu kiweke kwenye maandishi, msikubali kushinikizwa kufanya mambo nje ya utaratibu na ni muhimu kwenu kuwa wabobezi ili iwe rahisi kutambua sheria inapokiukwa.”

Waziri ameitaka Takukuru kuanzisha madawati kuangalia kwa kina miradi ya maendeleo katika kila taasisi ya ununuzi na kufuatilia uendeshaji wake.

Mwenyekiti wa CoST, Mhandisi Kazungu Magili amesema uwazi katika miradi unachangia kwa kiasi kikubwa kuchochea uwajibikaji.

Amesema kuficha taarifa katika miradi kunasababisha kuwepo minong’ono na hasa inayohusisha harufu ya rushwa.

“Ili kuondoa minong’ono ni vyema taarifa za miradi kuwekwa wazi kinyume cha hapo itahesabika kuwa kuna mchezo mchafu ndani yake ikiwemo rushwa na ufisadi. Sisi kazi yetu ni kuhamasisha uwazi na uwajibikaji, hatuhusiki na ukaguzi wala kumtafuta mchawi hivyo tunasisitiza taasisi za ununuzi zishirikiane nasi katika utendaji wetu wa kazi,” amesema.