Kiwanga, Lijualikali na wenzao wapelekwa rumande

Mbunge wa jimbo la Kilombero, Peter Lijualikali akifurahia jambo akiwa ndani ya gari na watuhumiwa wenzake 35 wanaotuhumiwa kuharibu mali katika kijiji cha Sofi wilaya ya Malinyi baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi mdogo wa marudio wa udiwani kata ya Sofi. Picha na Juma Mtanda.

Muktasari:

Wakili Kibatala amesema kuahirishwa kesi na kutotolewa dhamana kwa washtakiwa kunalenga kuchelewesha upatikanaji wa haki.

Morogoro. Maombi ya dhamana ya wabunge wawili wa Chadema na washtakiwa wengine 37 yamekwama kusikilizwa ikielezwa hakimu anaumwa. 

Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, imeelezwa hakimu Ivan Msack anayesikiliza kesi hiyo ni mgonjwa hivyo imeahirishwa na washtakiwa wamepelekwa rumande hadi Desemba 8,2017.

Akiahirisha kesi hiyo leo Jumatano Desemba 6,2017, hakimu Erick Rwehumbiza amesema Msack amepata maradhi ghafla na yuko hospitalini kwa matibabu. 

Baada ya kuelezwa mahakamani kuwa hakimu ni mgonjwa, upande wa utetezi ulimuomba Rwehumbiza kesi hiyo ihamishiwe kwa hakimu mwingine. 

Wakili wa utetezi, Peter Kibatala amesema kuahirishwa kesi hiyo na kutotolewa dhamana kwa washtakiwa kunalenga kuchelewesha upatikanaji wa haki. 

Kibatala pia ameiomba Mahakama iruhusu wananchi kuingia ndani ya ukumbi kufuatilia uendeshaji wa kesi hiyo.

Wakili wa Serikali, Sunday Hyera akizungumzia hoja ya wananchi kuruhusiwa kuingia ndani ya ukumbi wa Mahakama amesema haina msingi katika kesi hiyo na hakuna uwezekano wa kuiwasilisha mahakamani. 

Hakimu Rwehumbiza akijibu hoja hizo, amesema alipewa jalada la kesi kwa ajili ya kuiahirisha.

Kuhusu dhamana amesema ombi hilo litashughulikiwa na hakimu anayehusika na iwapo hatakuwepo Desemba 8,2017 wataangalia namna ya kuihamishia kwa hakimu mwingine.

Hakimu Rwehumbiza amesema suala la wananchi kuingia mahakamani haliathiri uendeshaji wa kesi kwa kuwa wanaweza kuwepo wawakilishi wao.

Wabunge Susan Kiwanga wa Mlimba na Peter Lijualikali wa Kilombero na washtakiwa wengine walifikishwa mahakamani Novemba 30,2017 wakidaiwa Novemba 26,2017 katika Kata ya Sofi wilayani Malinyi walifanya uharibifu wa mali.

Wanadaiwa bila uhalali, huku wakijua wanatenda kosa walikula njama na kuchoma moto ofisi ya kata na kufanya uharibifu wa mali.

Hakimu alisema angetoa uamuzi wa dhamana jana Desemba 5,2017 lakini hilo halikufanyika kutokana na kuibuka hoja za kisheria kuhusu hati ya kiapo ya kupinga dhamana iliyowasilishwa mahakamani hapo.

Kutokana na mvutano wa kisheria, hakimu Msack aliahirisha kesi hiyo hadi leo Jumatano Desemba 6,2017 ili kutoa fursa kwa pande zote mbili kujibu hoja kuhusu hati hiyo.