Thursday, October 12, 2017

Ugonjwa wa kisukari watajwa kusababisha upofu wa macho

 

By Fortune Francis, Mwananchi ffrancis@mwananchi.co.tz

Msimamizi Mkuu wa Hospitali ya Kimataifa ya Macho (IFG), Adam Mwatima amesema ugonjwa wa kisukari umechangia watu wengi kupata upofu.

Mwatima alisema kuwa watu wengi waliopata ugonjwa huo wameathirika macho, hivyo wanalazimika kwenda nje ya nchi kutibiwa jambo ambalo linawagharimu fedha nyingi.

Alisema kutokana na ugonjwa huo kukithiri nchini, hospitali hiyo inatoa huduma ya upasuaji ili kupunguza gharama za matibabu na usafiri wa kwenda nje.

Mwatima alisema madaktari bingwa kutoka Bara la Ulaya watafanya upasuaji kwa wagonjwa hao wakiwamo waliopata presha ya macho na kisukari cha macho, lengo ni kuhakikisha wanapatiwa matibabu kabla ugonjwa huo haujawaathiri na kuwaletea upofu wa maisha.

“Siku ya upofu duniani inaadhimishwa Oktoba 12 na Nyerere Day itakuwa Oktoba 14, siku hiyo tutatoa huduma kwa punguzo la asilimia 25 kwa huduma zote za macho ikiwamo upasuaji,” alisema Mwatima.

Pia, alisema hospitali ipo tayari kuingia mkataba na Serikali ili kutoa mafunzo kwa madaktari wa macho ambayo yatatolewa na madaktari bingwa kutoka nje.

Mmoja wa wagonjwa wanaotibiwa kwenye hospitali hiyo, Innocent Ibrahim alisema awali huduma kwa wagonjwa waliopata kisukari cha macho ilikuwa inatolewa nje ya nchi, ikiwamo India ambayo gharama ya matibabu zilikuwa juu.

“Tunashukuru kwa huduma hii kwa kuwa itatusaidia watu wenye uwezo mdogo, mfano ukigundulika una matatizo ya presha na kisukari cha macho awali huduma yake ilikuwa inatolewa nje ya nchi lakini kwa sasa tutaipata nchini,” alisema Ibrahim.     

-->