Ugumu wa dhamana wamkwaza Jaji

Muktasari:

Asema baadhi ya mahakimu hutumia masharti magumu kwa washtakiwa

Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu amesikitishwa na ugumu wa upatikanaji wa dhamana kwa washtakiwa wa makosa mbalimbali kisiwani Pemba.

Makungu alisema hayo juzi kwa nyakati tofauti, alipozungumza na watendaji wa mahakama za mwanzo Wingwi, Konde na Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Alisema anashangaa kuona baadhi ya mahakimu wanatumia masharti magumu kwa washtakiwa ili waendelee kusota mahabusu wakati makosa wanayoshtakiwa yana dhamana.

Makungu alisema lazima mahakimu wafahamu kuwa kumpeleka mtuhumiwa rumande ni hatua ya mwisho na si kipaumbele chao.

“Sasa naambiwa masharti makubwa yanayotumika ili uweze kupewa dhamana uwe na wafanyakazi wawili wa Serikali na barua ya Sheha jambo ambalo wakati mwingine ni gumu kulitekeleza,’’ alisema Jaji Makungu.

Alifafanua kuwa hajaona popote kwenye sheria, mtuhumiwa anatakiwa ili kutimiza masharti awe na mtu anayefanya kazi serikalini au apate barua ya Sheha vinginevyo apelekwe rumade.

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu huyo alisema Mahakimu lazima wafanye kazi kisayansi na si kwa mashindikizo ya wanasiasa, maana wakifanya hivyo watakuwa hawaitendei haki fani yao.

Mrajis wa Mahakama Kuu Zanzibar; Mohamed Ali Mohamed alisema sasa watakuwa makini kwa mahakimu watoro na wanaopenda kusafiri bila ya dharura maalumu.

“Wapo mahakimu unawaona Unguja mara kwa mara bila ya safari maalumu za kikazi na huku wameziacha kesi juu ya meza na kuwatia watu tabu, sasa hawa tutapambana nao,” alisema.

Mrajisi wa Jimbo Mahakama Kuu Pemba, Hussein Makame Hussein, alisema changamoto kadhaa wamezisikia ikiwamo kucheleweshewa mienendo ya kesi, jambo ambalo kwa sasa wanajitahidi kulishughulikia.