Ugumu wa maisha Dodoma kikwazo Dodoma

Muktasari:

Ombi hilo lilitolewa juzi na Mwenyekiti wa Mtaa wa Mtube, John Masaka ambaye alisema wakazi wa Muungano hawawezi kuyafurahia makao makuu kutokana na umaskini walionao.

Dodoma. Serikali imetakiwa kuingilia kati suala la ugumu wa maisha na maboresho ya makazi kwa wananchi wa Mtaa wa Muungano Manispaa ya Dodoma ili waweze kuyafurahia makao makuu.

Ombi hilo lilitolewa juzi na Mwenyekiti wa Mtaa wa Mtube, John Masaka ambaye alisema wakazi wa Muungano hawawezi kuyafurahia makao makuu kutokana na umaskini walionao.

Masaka alisema maisha ya wakazi wengi wa Muungano yanategemea misaada na wengine huendesha maisha yao kwa kuokota katika jalala la taka la Mwanga.

Masaka alisema kwa muda mrefu watu hao wamekuwa na maisha magumu ambayo ni vigumu kuyaeleza na kama hawamo katika maandalizi ya mji mkuu Serikali ifahamu kwamba tatizo la ombaomba halitakwisha.

“Hawa watu hawawezi kuyaona makao makuu kama ni mkombozi kwao, badala yake yatakuwa ni mateso zaidi kwani gharama za maisha zitapanda na wao kuzidi kudidimia katika dimbwi la umaskini,” alisema Masaka.

Kiongozi huyo aliitaka serikali ya wilaya na mkoa kuingilia kati suala hilo ili kuyanusuru maisha ya wakazi hao.

Akikabidhi msaada wa chakula na vitu vingine, Miss Dodoma 2016, Anna Nitwa aliwaomba watu wenye uwezo kuingilia kati suala hilo kwa kufanya jitihada za makusudi kuboresha maisha ya watu wa Muungano ili wawe sehemu ya makao makuu.

Anna aliwapelekea msaada wa chakula na nguo wajane na watoto yatima waishio Muungano.