Uhaba wa damu salama unavyoondoa uhai wa wajawazito 500 nchini

Muktasari:

Ofisa huyo alisema asilimia 40 ya vifo hivyo vingeweza kuepukwa kama kungekuwa na akiba ya damu inayotosha katika hospitali.

Wajawazito wanapokwenda kujifungua hukumbana na changamoto nyingi ikiwamo huduma, vifaa tiba, dawa na damu salama.

Wakati changamoto hizo kila moja ina mchango wake katika ufupishaji wa maisha ya mama na mtoto anayetarajiwa kuzaliwa, damu pekee imetajwa kuondoa uhai wa zaidi ya wanawake 550 kati ya 100,000 wanaokwenda kujifungua hospitali. Kwa mujibu wa mkuu wa kitengo cha uhamasishaji na uhusiano cha Damu Salama, Rajabu Mwenda idadi hiyo ya akinamama hupoteza maisha kutokana na uhaba wa damu ya kuongezwa miilini.

Ofisa huyo alisema asilimia 40 ya vifo hivyo vingeweza kuepukwa kama kungekuwa na akiba ya damu inayotosha katika hospitali.

Mwenda alisema lita 450,000 zinahitajika kila mwaka kukabiliana na uhaba wa damu nchini.

“Ni jukumu la kila Mtanzania kujitolea kuchangia damu katika vituo vilivyo karibu yao ili kukomesha vifo ambavyo vinasababishwa na ukosefu wa damu,” alisema.

Aliongeza kuwa katika kipindi cha robo mwaka cha Julai hadi Septemba ofisi ya Mpango wa Taifa wa Damu Salama imekusanya chupa za damu 58,466 kutoka vikundi mbalimbali ikiwamo madhehebu ya dini.

Mkazi wa Tabata, Julius Michael aliwataka wananchi kuendelea kuchangia damu huku akiwataka viongozi wa Serikali kuligeuza suala la uchagangiaji wa damu kuwa ajenda yao wanapokuwa majukwaani kama walivyowahi kufanya miaka ya nyuma kuhusu Ukimwi.