Uhalifu mpakani wawatesa Karagwe

Muktasari:

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Muguruka, Kata ya Bweranyange ulioitishwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Godfrey Mheluka, wakazi  hao walisema uhalifu umekithiri katika maeneo hayo na kuhatarisha usalama wa maisha yao.

Karagwe. Wakazi wa vijiji vya Muguruka na Chamchuzi wilayani hapa, Mkoa Kagera wameiomba Serikali kuimarisha ulinzi wa mpaka wa Tanzania na Rwanda kwenye mwalo wa Rukombe na vijijini vilivyopo pembezoni mwa mto Kagera kutokana na kukithiri kwa  uhalifu.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Muguruka, Kata ya Bweranyange ulioitishwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Godfrey Mheluka, wakazi  hao walisema uhalifu umekithiri katika maeneo hayo na kuhatarisha usalama wa maisha yao.

Ofisa Elimu wa Kata ya Bweranyange,  Godwin Mbeikya alisema tangu mwaka 1972 Watanzania waliouawa kwa kupigwa risasi kutokana na vitendo vya uhalifu ni 56, kati ya  hao, 20 ni wa Kijiji cha Muguruka na wengine Chamchuzi.

Mkazi wa kijiji hicho, Dominick Benjamini (41), alisema ulinzi kwenye mwalo wa Rukombe na vijiji vya Mubari, Kisayo, Mto Kagera na Kizinga ni muhimu kwani hata inapotokea Mtanzania kwenda maeneo hayo hupigwa risasi na watu wanaojifanya ni askari wa doria wa Rwanda.

Mkuu wa wilaya Mheluka alipiga marufuku mwananchi yeyote kuvua samaki katika Ziwa Ihema, kwani halipo Tanzania na kuwataka kuacha kuendelea na shughuli za uvuvi katika mto Kagera na visiwa vingine mpaka Serikali itakaponunua boti za kuimarisha ulinzi.