Tuesday, August 8, 2017

Uingizaji wa bidhaa kutoka Kenya waporomoka

By Mwandishi Wetu, Mwananchi mwananchi@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Usafirishaji wa bidhaa za Kenya kuja Tanzania umeporomoka kwa asilimia 34 katika kipindi cha miezi mitano, ikiwa ni kiashiria cha matokeo hasi ya vizuizi vinavyowekwa kwenye biashara.

Biashara imeporomoka kwa Ksh4.35 bilioni (sawa na Sh87 bilioni) hadi Ksh8.2 bilioni (Sh164 bilioni) mpaka kufikia Mei mwaka huu, ikilinganishwa na Ksh12.55 bilioni (Sh251  bilioni) zilizorekodiwa katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Takwimu ya Kenya (KNBS), usafirishaji wa bidhaa kwenda Uganda umeendelea kukua na kuimarisha nafasi ya nchi hiyo katika bidhaa zinazozalishwa viwandani.

Kwa upande mwingine, Tanzania imekuwa kwenye mgogoro wa muda mrefu wa kufikia masoko ya Kenya, mgogoro ulioongezeka zaidi Mei baada ya Tume ya Udhibiti wa Nishati ya Kenya kupiga marufuku kuingizwa kwa gesi nchini humo kupitia mpaka wa Namanga kwa kile walichodai ni sababu za ubora.

“Tanzania imekuwa ikiuza gesi ya LPG kwa zaidi ya miaka 10. Biashara hii imeimarika sana. Tumewekeza na tunazidi kuwekeza kwenye miundombinu ili kuhakikisha kwamba tunaimarisha soko la pamoja la Afrika Mashariki,” inasomeka sehemu ya taarifa ya wafanyabiashara nchini hapa.

Hata hivyo, Tanzania ilijibu mapigo kwa kuzuia uingizwaji wa maziwa na sigara kutoka Kenya.

-->