Ujasiri wampandisha ndege ‘Tisekwa Shujaa’

Joseph Pesambili ambaye ni baba mzazi wa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Butwa, Geita, Tisekwa Gamungu (16), akionyesha hati ya ujasiri aliyokabidhiwa mwanaye na Taasisi ya Maafa na Uokoaji ya Suleiman Kova, Dar es Salaam jana. Picha na Bakari Kiango

Muktasari:

Mei 22: Siku ambayo tukio lilitokea baada ya kumaliza mtihani wa muhula wa kwanza.

30: Idadi ya wanafunzi ambao huvuka kila siku kwenda kwenye shule hiyo iliyopo Kisiwa cha Butwa.

Mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Butwa wilayani Geita, Tisekwa Gamungu amezungumzia namna alivyofanikiwa kuwaokoa wenzake tisa waliokuwa wamezama Ziwa Victoria.

Tisekwa ambaye alisafirishwa hadi jijini Dar es Salaam kwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATC) kukutana na wadau mbalimbali ambao walimpatia pongezi sambamba na zawadi ya Sh1.9 milioni na cheti cha ushujaa, alisema siku aliyowaokoa wenzake alifanya kazi ngumu lakini yenye mafanikio.

Katika safari hiyo ambayo imekuwa ya mafanikio kwa Tisekwa baada ya kuzawadiwa na kutunukiwa cheti cha ushujaa, mwanafunzi huyo aliambatana na baba yake mzazi, Joseph Pesambili.

Tisekwa (16) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano Shule ya Msingi Butwa, alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi 12 walionusurika baada ya mtumbwi waliopanda kupigwa na mawimbi na kusababisha vifo vya wenzao wawili.

Akizungumza na gazeti hili jana baada ya mahojiano na kipindi cha 360 kinachorushwa na Televisheni ya Clouds, Pesambili alisema anaona kama ndoto kupanda ndege.

“Kweli sikufikiria katika maisha yangu kama nitapanda ndege. Hii ni kama ndoto kati yangu na mwanangu Tisekwa, nawashukuru wote waliofanikisha safari hii,” alisema Pesambili ambaye alionekana mwenye furaha wakati wote.

Mtayarishaji wa kipindi cha 360, Dotto Bahemu alisema Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ni miongoni mwa wadau waliofanikisha safari Tisekwa ambalo limetoa tiketi za kuja Dar es Salaam na kurudi Mwanza.

Mkurugenzi wa Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi alisema shirika hilo liliamua kuungana na wadau kufanikisha safari ya Tisekwa kutokana na kazi kubwa aliyoifanya. “Mtoto mdogo kuokoa wenzake siyo jambo dogo,” alisema Matindi.

Kwa mujibu wa Mratibu Elimu Kata ya Izumachel, Thom Samson zaidi ya wanafunzi 30 huvuka kwa kutumia boti na mitumbwi kila siku kwenda na kurudi shule ya msingi Butwa.

Wanafunzi waliopoteza maisha kutokana na kuzama katika ziwa hilo ni Kumbuka Bruno (13) wa darasa la tano, Anastazia Christopha (12) wa darasa la tatu na Sophia Muungano (11) darasa la pili. Wote walizikwa pembezoni mwa ziwa hilo kama mila na tamaduni za watu wa eneo hilo.