Ujenzi maktaba kubwa kuliko zote Afrika mbioni kukamilika

Muktasari:

  • Ujenzi wake unaendelea Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM).

 Ujenzi wa maktaba ya kisasa na kubwa kuliko zote barani Afrika unaondelea katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa Sh90 billioni, umekamilika kwa asilimia 90 na unatarajiwa kukabidhiwa Julai, 2018.

Hayo yamebainishwa leo Februari 9, 2018  wakati wa ziara ya Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako na Balozi wa China nchini, Wang Ke ambao walitembelea UDSM kuojionea maendeleo ya mradi huo unaojengwa kwa msaada wa Serikali ya China.

Waziri Ndalichako amesema ujenzi huo wa maktaba yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,100 kwa wakati mmoja na kuhifadhi vitabu laki nane utakamilika mapema Julai, 2018 na mbali na kusaidia masomo utavutia utalii nchini kwa watu kuja kujifunza mambo mbalimbali.

"Nimeona jengo hili linakaribia kukamilika lipo tayari kwa karibu asilimia 90, vitu vyote muhimu vipo tayari kilichobaki ni kumaliza tu," amesema Ndalichako.

Amesema ujenzi wa maktaba hiyo umezingatia wanafunzi wenye mahitaji maalumu (walemavu) pamoja na tatizo la kukatika kwa umeme ambalo limewekewa mfumo wa sola kwaajili ya taa na viyoyozi.

Balozi wa China,  Ke amesema anafurahi kuona maendeleo mazuri ya ujenzi wa jengo hilo ikiwa ni miezi 20 tangu Rais John Magufuli aweke jiwe la msingi, na maendeleo hayo ni kutokana na ushirikiano baina ya wataalamu wa Tanzania na Uchina.

"Nafurahi kuona ujenzi unakaribia kumalizika lakini hii ni matokeo ya ushirikiano wa kina kati ya wafanyakazi wa China na Tanzania, wote kwa pamoja wamejibu wito wa Rais Magufuli wa hapa kazi tu," amesema Ke.

Pia,  Ke amewatakia heri ya mwaka mpya wa Kichina wafanyakazi wanaotekeleza mradi huo na Watanzania wote.

 Siku hiyo muhimu kwa Wachina wote ulimwenguni inatarajiwa kuadhimishwa siku sita zijazo.

Makamu mkuu UDSM, Profesa William Anangisye amesema kukamilika kwa maktaba hiyo unaongeza ukubwa na hadhi ya chuo katika suala zima la taaluma.

"Maktaba ya zamani iliyojengwa mwaka 1964 hadi mwaka 1965 ambayo mpaka sasa ni kubwa katika ukanda huu itaendelea kuwapo kwa ajili kumbukumbu za zamani hii itawekewa vitabu vipya zaidi," amesema Profesa Anangisye.