Ujenzi reli ya kisasa sasa wachanja mbuga

Muktasari:

Reli hiyo itatumiwa na treni yenye kasi ya kilomita 160 kwa saa na uendeshaji wake utakuwa wa umeme au mafuta.

Kibaha. Ujenzi wa awamu ya kwanza wa reli ya kisasa (SGR), umefikia asilimia 16, ukitarajiwa kukamilika Novemba 2019.

Reli hiyo itatumiwa na treni yenye kasi ya kilomita 160 kwa saa na uendeshaji wake utakuwa wa umeme au mafuta.

Mkuu wa mipango wa kampuni ya Yapi Merkezi, Enis Eryilmaz alisema hayo jana katika eneo la Soga wilayani Kibaha mkoani Pwani alipozungumza wakati wa ziara ya Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini (ERB).

Eryilmaz alisema kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro chenye urefu wa kilomita 300 kitakuwa na vituo sita vya Dar es Salaam, Pugu, Soga, Ruvu, Ngerengere na Morogoro.

“Tumejipanga kumaliza mradi huu ndani ya wakati, tunatumaini tutasherehekea uzinduzi Novemba 2019,” alisema mtaalamu huyo.

Alisema wanafanya kazi usiku na mchana, lakini changamoto kubwa ni mvua nyingi inaponyesha.

Mtaalamu huyo alisema kampuni imeajiri watu 4,000, kati yao Watanzania ni asilimia 90.

“Tunajitahidi kufanya kazi bega kwa bega na Watanzania ili tukiondoka waweze kuendesha mradi huu na kufanya matengenezo mengine,” alisema.

Alisema Agosti wataanza kulaza mataruma kwenye baadhi ya maeneo wanayoyajenga.

Meneja mradi msaidizi kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC), mhandisi Machibya Masanja alisema reli hiyo itakuwa na kituo cha kupoza umeme kila baada ya kilomita 50 na Shirika la Umeme (Tanesco) litaweka umeme maalumu kwa ajili ya reli hiyo.

Alisema Dar es Salaam itakuwa na treni maalumu kwa abiria na watajenga kituo kikubwa eneo la Pugu kwa ajili ya abiria wa Dar es Salaam na waendao mikoani.

Awali, mwenyekiti wa ERB, Profesa Ninatubu Lema aliiomba kampuni hiyo kuchukua makandarasi wanafunzi kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo mbinu na teknolojia za uhandisi.

Profesa Lema alisema mradi wa SGR ni mkubwa na kwa nchi kama Tanzania hutokea mara moja ndani ya miaka 100.

“Tumefurahi kuona kazi inafanyika kwa umakini mkubwa wa kiuhandisi na wana vifaa vya kisasa. Pia, tumefurahi kuona Watanzania wanashirikishwa lakini kwa (kiwango) level ya wahandisi bado wako wachache,” alisema.

Awali, mkoani Dar es Salaam, meneja mradi wa ujenzi wa reli hiyo, Young-Hak Choi aliishauri Serikali kutengeneza sheria maalumu itakayosimamia miradi mikubwa.

Alisema sheria zilizopo zinawataka makandarasi kulipa tozo ya mitambo inayoingizwa nchini, hivyo kuwapo uwezekano wa kuchelewesha kukamilika miradi.

Choi alisema reli ya kisasa ni muhimu kwa Watanzania na ni vyema sheria zinazokwamisha mradi huo zikaondolewa.