Tanzania yafikia asilimia 16 ujenzi reli ya kisasa

Muktasari:

Mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba mwakani


Dar es Salaam. Ujenzi wa awamu ya kwanza wa reli ya kisasa (Standard Gorge) umefikia asilimia 16 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 30 ifikapo Novemba 2019.

Reli hiyo ya kisasa itakuwa ya treni yenye kasi ya kilomita 160 kwa saa na uendeshaji wake utatumia umeme au mafuta.

Akizungumza leo Julai 17 wakati wa ziara ya Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Mkuu wa Mipango (Planning Chief) wa kampuni ya Yapi Merkezi, Enis Eryilmaz amesema kipande cha Dar - Morogoro chenye kilomita 300 kitakuwa na vituo sita ambavyo ni Dar, Pugu, Soga, Ruvu, Ngerengere na Morogoro.

"Tumejipanga kumaliza mradi huu ndani ya wakati, tunatumaini tutasherehekea uzinduzi wake Novemba 2019," amesema mtaalamu huyo.

Eryilmaz amesema wamekuwa wanafanya kazi usiku na mchana lakini changamoto kubwa tuliyokabiliana nayo ni mvua nyingi zinaponyesha.

Amesisitiza kwamba kampuni ya Yapi Merkezi imeajiri watu 4000, kati yao Watanzania ni asilimia 90. Amesema ushiriki wao ni mzuri na wengi wanafanya kazi vizuri.

"Tunajitahidi kufanya kazi bega kwa bega na Watanzania ili tukiondoka waweze kuendesha mradi huu na kufanya matengenezo mengine," amesema.

Amebainisha kwamba ifikapo Agosti, mwaka huu wataanza kulaza mataluma ya reli kwenye baadhi ya maeneo wanayojenga.

Meneja mradi msaidizi kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Machibya Masanja amesema reli hiyo itakuwa na kituo cha kupoza umeme kila baada ya kilomita 50 na Shirika la Umeme (Tanesco) litaweka umeme maalumu kwa ajili ya reli hiyo.

Amesema Dar es Salaam itakuwa na treni maalumu kwa abiria na watajenga kituo kikubwa Pugu ambacho kitakuwa kinapakia abiria wa Dar es Salaam na waendao mikoani.

Awali akizungumza na wakandarasi hao, mwenyekiti wa ERB, Profesa Ninatubu Lema amewaomba kuchukua wakandarasi wanafunzi kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo mbinu na teknolojia mbalimbali za uhandisi.

Amesema mradi wa SGR ni mkubwa na kwa nchi kama Tanzania, hutokea mara moja ndani ya miaka 100.

"Tumefurahi kuona kazi inafanyika kwa umakini mkubwa wa kihandisi na wana vifaa vya kisasa. Pia, tumefurahi kuona watanzania wanashirikishwa lakini kwa level ya wahandisi bado wako wachache," amesema Profesa Lem