Ujenzi wa kiwanda wawakuna wabunge

Muktasari:

Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, iliyotembelea mradi huo jana, ilipongeza namna mifuko ya hifadhi ya jamii ya NSSF na PPF inavyotekeleza mradi huo.

 Hatua ya ujenzi wa kiwanda cha sukari kwenye gereza la Mbigiri mkoani Morogoro kupitia kampuni Hodhi ya Mkulazi Holding kwa ushirikiano na Magereza, unaonekana kuwafurahisha wabunge.

Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, iliyotembelea mradi huo jana, ilipongeza namna mifuko ya hifadhi ya jamii ya NSSF na PPF inavyotekeleza mradi huo.

Pia, wabunge hao walionyesha kuridhishwa zaidi na namna mradi huo unavyohusisha wananchi waliopo jirani ambao mbali na kupata ajira za moja kwa moja, wamepatiwa fursa ya kulima miwa ili kukiuzia kiwanda hicho.

“Baada ya kusikiliza mpango mikakati kisha kutembelea shamba kwa kweli kamati imeridhishwa namna wadau hawa wanavyotekeleza mradi huu,” alisema mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohamedi Mchengelwa na kuongeza:

“Inaonyesha ulifanyika utafiti wa kutosha kabla na matunda yake kiukweli yameanza kuonekana, kikubwa tu tunachowaomba wamalize kwa wakati.”

Akijibu baadhi ya hoja za wabunge hao ambao pia walitaka kufahamu uwezekano wa mifuko hiyo kuwekeza kwenye sekta ya uvuvi nchini, waziri wa ajira, Jenista Mhagama alisema uwezekano huo upo ikiwa mamlaka zinazosimamia mifuko hiyo zitaridhia kwa kuangalia vigezo muhimu.

Naye mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Mkulazi ambaye pia ni mkurugenzi mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara alisema kufikia mwakani mradi huo utakuwa umekamilika.

“Mradi huu mliotembelea unalenga kuzalisha tani 50 za sukari kwa mwaka, na ni sehemu tu ya mradi mkubwa unaotekelezwa na mifuko yetu miwili yaani NSSF na PPF ukiwapo mwingine mkubwa zaidi katika eneo la Ngerengere, Wilaya ya Morogoro Vijijini unaofahamika kama Mkulazi I,” alisema.

Naye mkurugenzi mkuu wa PPF, William Erio alisema wamelenga soko la ndani na nje, huku akiahidi mradi huo kukamilika kabla ya wakati uliopangwa.