Ujerumani yatoa ipad 40 shule ya msingi Makuyuni

Mkurugenzi wa Mji wa Kiel ,Ujerumani  Sebastian Schneider akikabidhi iPads kwa  wanafunzi wa shule ya Msingi Makuyuni, iliyopo Mji mdogo wa Himo,Wilaya ya Moshi. Picha na Janeth Joseph.

Muktasari:

Schneider amesema msaada huo una nia ya kuimarisha mshikamano na ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Ujerumani uliodumu kwa miaka mingi sasa.


Himo. Serikali ya Ujerumani imetoa msaada wa Ipad 40 zenye thamani ya Sh25 milioni   kwa wanafunzi wa shule ya msingi Makuyuni ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora.

 Akikabidhi msaada huo jana Agosti 20 Mkurugenzi wa shirika la Ujerumani la Deacon, Sebastian Schneider amesema nia ya kutoa ipad hizo ni kuhakikisha wanafunzi wanaendana  na elimu ya kisasa ya sayansi na teknolojia.

Pia amesema msaada huo una nia ya kuimarisha mshikamano na ushirikiano uliopo baina ya Tanzania  na Ujerumani uliodumu kwa miaka mingi sasa.

 “Nimetoa msaada huu kwa sababu mimi ninafanya kazi na vijana na pia ninapenda kuona watoto wakifanya vizuri katika masomo yao, hivyo tumetoa fedha pamoja na ipads na lengo  ni kuinua elimu kwa watoto hawa wa Tanzania,”amesema Schneider.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Michael Kilawila alimpongeza mfadhili huyo kwa kujitolea kusaidia shule hiyo kwani itawasaidia wanafunzi kufanya vizuri kitaaluma.

Kilawila amesema msaada huo ni mkubwa hivyo alimtaka Mkuu huyo wa shule kuhakikisha Ipad hizo zinatunzwa vizuri ili ziwasaidie watoto hao katika kuhakikisha wanafanya vizuri katika masomo yao.

“Ni msaada mkubwa kwa watoto hawa hasa katika dunia hii ya sayansi na teknolojia, hivyo walimu na wazazi mshirikane kwa pamoja kuzitunza lakini pia kuhakikisha mnatafuta mtaalamu kwa ajili ya kuwafundisha watoto hao ili zisije zikabaki mapambo kwenye ofisi ya mkuu wa shule”amesema Kilawila.

Kwa upande wake Mkuu wa shule hiyo  Dorcus Mosha amesema kwa awamu hii ya sayansi na teknolojia Ipad hizo zitawasaidi kufundishia masomo mbalimbali  na kupanua ufahamu wao.

“Ni furaha kubwa na ya pekee kupata msaada huu mkubwa wa Ipad 40, hivyo tunaahidi kuzitunza na kuziweka katika mazingira mazuri ilizitumike kwa vizazi na vizazi hasa katika suala zima la ufundishaji wa kisasa.”amesema Mwalimu Mosha.