Ukaguzi magari binafsi kuanza Machi Mosi

Hamad Masauni, naibu waziri wa Mambo ya Ndani

Muktasari:

Mwenyekiti wa baraza hilo, Hamad Masauni alisema hayo jana alipotoa tathmini ya utekelezaji wa mpango mkakati wa awamu ya pili ulioanza Julai hadi Desemba mwaka jana ukilenga kupunguza ajali nchini.

Dar es Salaam. Baraza la Taifa la Usalama Barabarani limesema Machi Mosi litaanza ukaguzi wa magari ya watu binafsi, huku likieleza kupungua kwa ajali.

Mwenyekiti wa baraza hilo, Hamad Masauni alisema hayo jana alipotoa tathmini ya utekelezaji wa mpango mkakati wa awamu ya pili ulioanza Julai hadi Desemba mwaka jana ukilenga kupunguza ajali nchini.

Masauni, ambaye ni naibu waziri wa Mambo ya Ndani alisema ukaguzi wa magari ya watu binafsi unafanyika baada ya magari ya usafirishaji, wanafunzi na mizigo kukamilika mwaka jana.

“Kuanzia Machi Mosi naomba wamiliki wa magari binafsi wayapeleke katika vituo vya polisi au maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ukaguzi utakaochukua miezi miwili. Baada ya ukaguzi magari haya yatapewa stika maalumu itakayotolewa kwa Sh3,000,” alisema.

Masauni alisema, “Mamlaka, mashirika, idara na taasisi za Serikali zenye wafanyakazi wenye magari wanaweza kuleta maombi ya wakaguzi wa magari ili mchakato huu ufanyike maeneo yao ya kazi.”

Alisema katika mchakato huo hakutakuwa na njia ya mkato kwa watu waliozoea kutoa fedha kwa wahusika bila magari kukaguliwa.

“Askari yeyote asikubali kutoa stika bila kujiridhisha, ikibainika atachukuliwa hatua za kisheria yeye na mmiliki wa gari husika kwa mujibu wa sheria ya usalama barabarani,” alisema Masauni ambaye pia ni mbunge wa Kikwajuni, Zanzibar.

Naibu waziri aliwakumbusha wamiliki wa magari ya biashara na mizigo ambayo hayajakaguliwa kuyapeleka kwa ukaguzi kwa kuwa Machi Mosi wataanza msako wa kuyakamata na wahusika watachukulia hatua za kisheria.

Alisema magari 82,208 yakiwamo ya biashara na mizigo yalikaguliwa na kati ya hayo 79,221 yalibainika kuwa mazima na kubandikwa stika.

Masauni alisema magari 2,987 yalibainika kuwa na dosari ambazo wamiliki walitakiwa kuzirekebisha na kuyarejesha kwa ukaguzi.

Katibu mtendaji wa baraza hilo, ambaye pia ni Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamanda Fortunatus Musilimu amewataka wamiliki wa magari kuyapeleka kwa ukaguzi badala ya kusubiri nini kitatokea baada ya muda kumalizika.

“Hakuna gari itakayopewa stika bila kukaguliwa, kama mambo hayo yalikuwepo ni huko nyuma si sasa. Tunakagua na ukikidhi vigezo unapata stika na mchakato huu unafanyika ili kuondoa barabarani magari mabovu,” alisema Kamanda Musilimu.

Kuhusu ajali kupungua, alisema kati ya Julai hadi Desemba mwaka jana zilipunguza kwa asilimia 43.

Alisema takwimu zinaonyesha katika kipindi hicho zilitokea ajali 2,683 zilizosababisha vifo 1,330 na majeruhi 2,748.

Masauni alisema katika kipindi kama hicho mwaka 2016 kulikuwa na ajali 4,704 zilizosababisha vifo 1,676 na majeruhi 4,299.

“Mchanganuo huu unaonyesha ajali 2,021 sawa na asilimia 43 zimepungua, kwa vifo 346 sawa na asilimia 21 na kupungua kwa majeruhi 1,551 sawa na asilimia 36. Kwa takwimu hizi malengo ya mkakati wa awamu ya pili wa kupunguza ajali umefanikiwa kwa asilimia 33,” alisema Masauni.