Ukaidi wa dereva waua watatu ajali ya basi K’jaro

Kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamisi Issah

Muktasari:

Kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamisi Issah alisema ajali hiyo ilitokea Mei 20 majira ya saa 2:00 usiku eneo la Same mjini karibu na kituo cha ukaguzi cha polisi.

Moshi. Watu watatu wamefariki dunia na wengine wanne kujeruhiwa, baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na gari jingine eneo la Same, barabara kuu ya Dar es Salaam-Arusha.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamisi Issah alisema ajali hiyo ilitokea Mei 20 majira ya saa 2:00 usiku eneo la Same mjini karibu na kituo cha ukaguzi cha polisi.

Issah alisema gari la kampuni ya Hai Express likitokea Dar es Salaamu kuelekea Arusha, liligongana uso kwa uso kwa uso na Fuso lililokuwa likitokea Kilimanjaro kuelekea Dar es Salaam.

Ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu watatu waliokuwa kwenye fuso na wanne walikuwa kwenye basi walijeruhiwa.

Akielezea mazingira ya ajali hiyo, kamanda Issah alisema basi la abiria likitokea Dar es Salaam lilipofika eneo la Same mjini lilisimamishwa na askari lakini dereva alipuuza na kuchepuka upande wa kulia ambako Fuso lilikuwa limesimama kisha kugongana uso kwa uso.

“Katika eneo ambalo ajali imetokea, kuna gari lilikuwa limeanguka na kulikuwapo na askari, basi la Hai Express lilipofika eneo lile lilisimamishwa na polisi,” alisema Issah na kuongeza:

“Ilikuwa ni moja ya njia za kuchukua tahadhari kwa kuwa mbele kulikuwa na magari yamesimama, lakini kwa ukaidi wa dereva aligoma kusimama na kuendelea, alipokata kulia ambako Fuso ilikuwa imesimama iliigongana uso kwa uso na kusababisha vifo.”

Aliwataja waliofariki dunia ambao walikuwa kwenye Fuso ni dereva na utingo wake ambao majina yao hayajafahamika na abiria aliyefahamika kwa jina la Mariwadha Dafulio, mwenye miaka kati ya 48 na 50, mkazi wa Msambiazi Korogwe mkoani Tanga.

Aliwataja majeruhi kuwa ni Kasim Athuman (75), Daniel Mugabe (26) mwanafunzi wa mwaka wa tatu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Zubeda Salum (26)na Lightness Joseph (45) ambao wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Same.

Kamanda Issah alisema dereva wa basi Alex Mpwepa, mkazi wa Dar es Salaam kwa sasa anashikiliwa na polisi kwa mahojiano.

Alisema baada ya mahojiano watamfikisha dereva mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Wakati huohuo, mtu mmoja ambaye ni mbeba mizigo ya watalii katika Mlima Kilimanjaro, Joachim Mariwa amefariki dunia baada ya kuanguka kwenye Kituo cha Stella na kuporomoka hadi korongoni wakati akipanda mlima huo.

Kamanda Issah alisema Mariwa alikuwa mkazi wa Rau Manispaa ya Moshi na kwamba, taarifa za kifo chake zilipatikana Mei 19 saa 3:00 asubuhi baada ya uongozi wa mlima kubaini kuwapo kwa tukio hilo. Hata hivyo, Issah hakufafanuzi iwapo kama alikuwa akipandisha mtalii au la.