Ukame kikwazo kilimo cha mpunga

Muktasari:

Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Mbarali, Job Mlomo alitoa ushauri huo mwishoni mwa wiki wakati wa maadhimisho ya siku ya mkulima wa mpunga iliyoandaliwa na Mradi wa Shirika la Maendeleo la Kiholanzi (SNV).

Mbarali. Wakulima wa mpunga wilayani hapa wameshauriwa kulima mazao yanayostahimili ukame yakiwamo muhogo na viazi vitamu ili kuepuka hasara inayoweza kujitokeza.

Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Mbarali, Job Mlomo alitoa ushauri huo mwishoni mwa wiki wakati wa maadhimisho ya siku ya mkulima wa mpunga iliyoandaliwa na Mradi wa Shirika la Maendeleo la Kiholanzi (SNV).

Mlomo alisema msimu huu siyo rafiki kwa mpunga kutokana na mvua kuwa chache hivyo ni vyema wakachukua tahadhari kwa kulima mazao yanayostahimili ukame ili kuwa na chakula cha akiba.

Wilaya ya Mbarali ni miongoni mwa zinazolima mpunga kwa wingi nchini, lakini ukame umesababisha wakulima kushindwa kuotesha mbegu na hadi sasa hawajapanda.

Awali, Kaimu Meneja wa mradi wa kilimo cha mpunga, Anthony Mhagama alisema waliandaa maadhimisho hayo ili kuwakutanisha wakulima wajadili hali ya hewa na kilimo cha zao hilo msimu huu.

Mhagama alisema ukame unaingia wakati wakulima wakiwa na shauku ya kulima mpunga kwa wingi na tayari maghala manane yalikarabatiwa kwa gharama ya Sh49 milioni.

“Tunachokifanya ni kuhakikisha tunaboresha mazingira, kuimarisha biashara za mazao wanayozalisha kwa kuwatafutia masoko na kuwapatia mitaji,” alisema.

Mshauri Msaidizi wa Kilimo, Nicholaus Johaness, alisema mradi huo umewafikia wakulima 38,000, huku lengo likiwa kuwafikia 45,000 ambao wanapatiwa elimu ya kilimo cha hifadhi na afya ya udongo kwa kutumia mashamba darasa.