Ukarabati kuziba nyufa majengo ya hosteli UDSM waanza

Muktasari:

  • Kiongozi wa Daruso alishikiliwa  polisi kwa kuhojiwa kutokana na kusambaa picha zikionyesha nyufa kwenye majengo ya hosteli.

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umeanza ukarabati wa mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) yenye ufa.

Taarifa za kuwepo nyufa hizo zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii usiku wa Desemba 3,2017 na baadaye ufafanuzi ulitolewa na TBA.

Uchunguzi uliofanywa na MCL Digital umebaini ukarabati umeanza, huku ikielezwa kuwa hauwaathiri wanafunzi wanaotumia mabweni hayo.

“Ukarabati umeanza, mafundi wanafanya kazi nje ya jengo kwa kuondoa plasta ili kuangalia tatizo liko wapi,” kimesema chanzo cha habari kilichozungumza na MCL Digital.

TBA iliyojenga majengo hayo ambayo bado yako katika usimamizi wake imeelezwa pia inaangalia dosari nyingine zilizopo.

Mtendaji Mkuu wa TBA, Mhandisi Elius Mwakalinga Desemba 4,2017 akizungumzia nyufa zilizoko kwenye jengo la Block A alisema hazina madhara na walizitarajia.

Alisema nyufa katika jengo hilo la hosteli ambalo ni kati ya sita yaliyopo Block A zimetokea eneo walilotarajia ambalo kitaalamu linajulikana (expansion joint) hivyo hazina madhara.

Mwakalinga alisema kwa kawaida udongo unaobeba jengo hutitia baada ya muda fulani, hivyo wakati wa ujenzi huacha nafasi kuliwezesha jengo kupumua bila kusababisha nyufa.

Mwakalinga alisema kuna makosa yalifanyika ya kuziba nafasi zilizoachwa (expansion joint) kwa kutumia saruji badala ya mbao au plastiki maalumu hivyo kuonyesha nyufa kwenye jengo hilo.

Kutokana na kusambaa kwa picha kuonyesha nyufa katika majengo hayo, mbunge wa serikali ya wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso), Kumbusho Dawson alishikiliwa na polisi kitengo cha makosa ya mtandao kwa kuhojiwa na baadaye aliachiwa.