Ukatili: Mtoto aingizwa kalamu sehemu za siri

Muktasari:

  • Chanzo cha ukatili dhidi ya mtoto huyo kujulikana ni bibi mzaa baba, Abijeli Kenneth aliyeshtuka baada ya kumuona mjukuu wake akiwa mnyonge na hawezi kukaa vizuri alipoitembelea familia hiyo wakati wa likizo, hivi karibuni.

Dar es Salaam. Wakati ongezeko la ukatili dhidi ya watoto linaonekana kushika kasi, mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka minane (jina tunahifadhi) amefanyiwa ukatili kwa kuchokonolewa na kalamu kwenye njia ya haja kubwa na kuvutwa uume mara kadhaa na mama wa kambo.

Licha ya kufanyiwa ukatili huo, mtoto huyo mkazi wa Tabata Kinyerezi wilayani Ilala amedai mama huyo (jina linahifadhiwa) amekuwa akimnyanyasa kwa kumpiga, kumfanyisha kazi kupita kiasi na kumpa chakula kidogo hasa baba yake akiwa safarini.

Ripoti ya Haki za Binadamu ya 2017, iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), inaonyesha matukio 13,457 ya ukatili dhidi ya watoto yaliripotiwa huku asilimia 85 yakiwa ya ubakaji na ulawiti.

Chanzo cha ukatili dhidi ya mtoto huyo kujulikana ni bibi mzaa baba, Abijeli Kenneth aliyeshtuka baada ya kumuona mjukuu wake akiwa mnyonge na hawezi kukaa vizuri alipoitembelea familia hiyo wakati wa likizo, hivi karibuni.

Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwao, Tabata - Segerea, Abijeli alisema baada ya kumbana mtoto huyo alieleza namna alivyokuwa anafanyiwa ukatili na mama yake.

Alisema awali alipobaini mtoto huyo anakaa upande alimuuliza, lakini kwa kuwa aliogopa kupigwa alilazimika kumpeleka sehemu nyingine.

“Ikabidi nimchukue hadi kwa mwanangu mwingine anayeishi Mabibo, alipoona kuwa yupo huru akasimulia ukatili aliokuwa anafanyiwa na mama yake,” alisema Abijeli.

“Niliogopa sana hasa aliposema mama alikuwa anamvuta sehemu za siri na kumuingiza kalamu sehemu za siri.”

Bibi huyo alisema ilibidi ampeleke mjukuu wake kujisaidia, lakini akagundua kuwa hana uwezo wa kurusha mkojo mbali kama ilivyo kawaida jambo lililompa hofu.

“Mara ya kwanza nilipoona hawezi kurusha mkojo nilishtuka nikaona huenda kwa sababu ni mchana, ilibidi nisubiri asubuhi nikampeleka tena nikashangaa mkojo unaanguka miguuni,” alisema bibi huyo.

Alisema baada ya mtu mwingine kujiridhisha na hali hiyo, alimpigia simu baba wa mtoto ambaye alishauri apelekwe hospitali kwa ajili ya uchunguzi.

“Tulipita polisi tukapewa PF3 kisha tukaenda Amana (hospitali), daktari alipompima mtoto akatupatia majibu ambayo sikuelewa yamesemaje,” alisema.

Aliporejesha majibu hayo polisi, iligundulika kuwa mjukuu wake alikuwa anafanyiwa ukatili huo, hivyo mama yake alikamatwa na kushikiliwa katika Kituo cha Polisi Stakishari.

Mkuu wa kituo hicho aliyejitambulisha kwa jina moja la Kasira, hakutaka kuzungumzia suala hilo akidai yeye si msemaji wa polisi.

Hata askari aliyekuwepo kwenye kitengo cha dawati la jinsia la kituo hicho naye alikiri tukio hilo kufikishwa hapo, lakini hakutaka kuzungumzia kwa undani wala kutaja jina lake. Hata hivyo Mwananchi lina nakala ya kesi hiyo kufunguliwa kituoni hapo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni hakupatikana kuzungumzia suala hilo, licha ya juhudi za kumsaka kuanzia juzi.

Simulizi ya mtoto

Mtoto huyo anayesoma darasa la pili alisema mama yake alikuwa akimfanyia ukatili mara nyingi. “Alikuwa ananipeleka bafuni na kuniingiza pen (kalamu) huku ananivuta ‘mdudu wangu’. Sikuwa naweza kumwambia baba kwa sababu aliniambia angenipiga,” alisema mtoto huyo.

Huku akilengwa na machozi, mtoto huyo alisema mama huyo alikuwa akimpa kazi nyingi za kufanya ikiwamo kuosha vyombo na kupiga deki nyumba japo wakati mwingine alikuwa amechoka.

“Wakati mwingine nilikuwa napewa chakula kidogo, nisiposhiba nikiomba nanyimwa. Hata watoto wake wakikosea ananipiga mimi,” alisema.

Alisema mama huyo alikuwa akimzuia kukaa karibu na baba yake, hivyo hakuweza kumweleza kila anachofanyiwa.

“Kuna siku mama alinikwangua na kisu mguuni, nikaumia, lakini baba alivyokuja nilimdanganya nimejikwaruza,” alisema huku akionyesha kovu mguuni.

Baba anasemaje?

Baba wa mtoto huyo, Moses Mkingami alisema ukatili aliofanyiwa mwanaye umemsikitisha, lakini awali hakujua lolote kutokana na kazi zake za kusafiri mara kwa mara.

Alisema kuna wakati alihisi kuwa mtoto huyo hana raha na anashindwa kutembea, jambo lililomsukuma kumpeleka hospitali.

“Majibu yalionyesha anaingiliwa, lakini hakumtaja anayemfanyia kitendo hicho. Mama yake alisema huenda ni wajomba zake nyumbani kwao walikuwa wanamfanyia hivyo,” alisema baba huyo.

“Ilikuwa ni miezi sita tu tangu nimchukue kwa mama yake, kwa hiyo niliamini huenda alifanyiwa hivyo siku za zamani. Nikajua kwa sasa yuko sehemu salama.”

Mkingami alisema mkewe alikuwa anazuia kukaa karibu na mwanaye. Hata hivyo hakufuatilia akijua ni mapenzi ya mama kwa mtoto. “Ila hakuwa na furaha, muoga na nilipomuuliza mtoto hakuniambia chochote kama anateswa. Kuna wakati akiitwa alikuwa anakuja kwa kukimbia,” alisema.

Baba huyo alisema mtoto huyo alikuwa akiishi kwa woga na alikuwa anasalimia mara kwa mara kutokana na hofu hiyo.

Alisema kuwa siku alipopigiwa simu kwamba mkewe ndiye alikuwa akimfanyia ukatili huo mtoto hakuamini hadi ripoti ya daktari ilipoonyesha amefanyiwa mara kadhaa. “Nilikuwa safarini siku nilipopigiwa simu kuhusu ukatili kwa mtoto wangu, niliporudi nilikaa wiki nzima ndani nikishindwa kabisa kufanya kazi,” alisema.

Hata hivyo alisema mkewe aliachiwa huru kwa dhamana na kwamba kwa sasa hayupo nyumbani kwa sababu ya usalama kwa kuwa wananchi wana hasira.

“Hata mimi sasa natembea kwa tabu kila mtu anaulizia hali ya mtoto, majirani wote wanajua kuhusu hilo,” alisema Mkingami.

Majirani wa familia hiyo walisema mtoto huyo alikuwa anateseka, lakini hawakujua kama alikuwa akifanyiwa ukatili huo.

Anipha Zuruga alisema mwanamke aliyemfanyia ukatili mtoto huyo anapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kufikishwa mahakamani.

“Hatua za kisheria zichukuliwe na haki itendeke kwa sababu amemuumiza mtoto bila hatia,” alisema.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Hospitali ya Amana, Suphian Mudolwa alisema wana taarifa za tukio hilo, lakini kulingana na taratibu za kazi hawawezi kutoa taarifa za mgonjwa.

Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na masuala ya kisaikolojia na makuzi ya watoto ya Repssi, Edwick Mapalala alisema mtoto anapoumizwa kwa kufanyiwa ukatili wowote anaumia kisaikolojia na huwa wanyonge.