Ukawa, CCM wafika pabaya, hawaongei

Mbunge wa Sumve, Richard Ndasa (kushoto) akijalibu kutaka kuzungumza na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (kulia) ambaye anazuiliwa na Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea ili asizungumze naye walipohudhuria kikao cha bunge mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Hatua hiyo ilikuwa dhahiri jana baada ya Ukawa kutangaza kuwa hawatashirikiana na wabunge wenzao wa chama tawala katika shughuli za kawaida za kijamii, kama vile michezo na kutumia kantini ya Bunge, wakisema wenzao wameanza kuwabagua.

Dodoma. Sakata la wabunge wa Ukawa kususa vikao vya Bunge vinavyoongozwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson limefika pabaya baada ya baadhi ya wawakilishi hao kuanza kutowasalimia baadhi ya wabunge wa CCM.

Hatua hiyo ilikuwa dhahiri jana baada ya Ukawa kutangaza kuwa hawatashirikiana na wabunge wenzao wa chama tawala katika shughuli za kawaida za kijamii, kama vile michezo na kutumia kantini ya Bunge, wakisema wenzao wameanza kuwabagua.

Mbali na kitendo hicho, wabunge hao pia walitoka kimyakimya bungeni baada ya Dk Tulia kuingia, lakini safari hii hawakufanya mbwembwe za kujiziba midomo kama walivyofanya juzi.

Jana asubuhi, wabunge wa CCM Richard Ndassa (Sumve) na Kangi Lugola (Mwibala) walieleza kutojibiwa salamu zao na wabunge wa Ukawa na kusema kuwa kitendo walichofanyiwa ni jambo la kusikitisha.

Ndasa alitoa ushuhuda kuwa jana saa 2.43 asubuhi kabla ya kikao alienda walipokuwa wamekaa wabunge wa Ukawa, Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Saed Kubenea (Ubungo) kwa lengo la kuwasalimia, lakini salamu yake haikupokewa.

Alisema baada ya kufika eneo hilo, Kubenea alimziba mdomo Msigwa kwa mkono ili asizungumze chochote.

Ndassa alisema jambo wanalolifanya wabunge wa Ukawa siyo jema na halina tija kufanywa na wawakilishi hao wa wananchi.

“Sisi ni wabunge, hivi inapofikia kususa kuongea na wabunge wenzako, hatima yake nini?” alisema.

“Mimi nilienda kuwasalimia kama kawaida ambavyo huwa tunafanya kwa wabunge awe CUF, CCM au Chadema, sasa unavyosusa una maanisha nini,” alilalamika Ndassa.

Alisema kitendo cha kutosalimia ni cha juu sana na kwamba iwapo Ukawa wanashauriwa na mtu basi inawapasa kuchuja mambo mengine, likiwamo hilo la kuwasusa wabunge wenzao.

Lakini, juzi Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia wakati anawaongoza wabunge wa Ukawa kutoka bungeni aliwatuhumu wabunge wenzao wa CCM kuwa wamekataa maridhiano ya mezani ili kulirudisha taifa pamoja.

Mbatia ambaye ni Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, alisema wameamua hadi kujitoa katika mitando ya kijamii kama Whatsapp ambayo wamo pia wabunge wa CCM.

Msigwa alieleza jana kuwa uamuzi waliofikia kutoshirikiana na wabunge wa CCM ni sahihi na akawatuhumu kushirikiana na Dk Tulia kukandamiza uhuru wa Bunge.

“Tumeona tujitenge kuongea nao kwa kuwa wanaleta utani kwenye mambo ya msingi ya taifa na tumeona tuonyeshe hisia zetu, labda itasaidia.

“Ni bora tuachane nao kwenye mahusiano ya kawaida tutaonana nao tu kwenye vikao,” alisema Msigwa aliyekuwa nje ya kantini akieleza kuwa amekuja kwenye kikao cha Kamisheni.

Hata hivyo, alipohojiwa watafanyaje kazi katika vikao vya kamati, alisema yenye ni mbunge na kuingia kuhoji kwenye vikao vya kamati ni kutimiza majukumu ya msingi ya kibunge na haimaanishi atakuwa na mahusiano ya kawaida.

Lugola aliliambia gazeti hili kuwa alisikitishwa jana baada ya kudai kuwa Mbunge wa Chadema (Viti Maalumu), Lucy Magereli hakumjibu salamu yake wakati wakiingia bungeni licha ya kumsalimia mara tatu na kuwa katika umbali mfupi wa kusikika.

“Kusalimia ni jambo la utamaduni wetu. Nilikuwa namsalimia mbunge wa kike wa Ukawa, lakini hakujibu. Lakini, nikajua ni sababu ya wao kufunga mdomo na plasta, nikamtania au kwa sababu ya plasta hujibu ili isije kudondoka hakuitikia,” alisema Lugola.

Alisema ameshtushwa na hali ilipofikia na hajui sababu za msingi za wabunge wa Ukawa kufanya vitendo hivyo, kinyume na udugu na utamaduni wa Watanzania.

Mbunge huyo machachari, alisema wabunge wa CCM hawajawakosea Ukawa na wala hawajawatukana na kuwafanyia vurugu, kama wana tatizo na Naibu Spika wasihamishie hasira zao kwa wasiohusika.

Alisema Ukawa wana milango mingi ya kufuatilia kama wana tatizo na kiti na walishapeleka shauri lao Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuwa wana matatizo na Naibu Spika, lakini kwa sasa wanapitia nje ya mfumo wa kikanuni.