Ukawa wamejifunza nini matokeo ya uchaguzi mdogo?

Wafuasi wa Ukawa wakifurahia kusaini makubaliano ya vyama vinavyounda umoja huo kwenye viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam mwaka 2014. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Katika uchaguzi mdogo wa udiwami uliofanyika Juni 16, 2013 CCM ilifanikiwa kushinda viti vya udiwani katika kata 16 huku Chadema ikiambulia viti sita vya udiwani kwenye kata 22.

Vyama vya siasa nchini vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimepata matokeo mabaya katika uchaguzi mdogo wa udiwani kwa kuambulia kiti kimoja, huku CCM ikizoa viti 18 kati ya viti 19 vya udiwani uliohitimishwa Januari 22, mwaka huu.

Kwa nini vyama hivyo havikufanya vizuri katika uchaguzi huo tofauti na Uchaguzi Mkuu mwaka 2015? Je, vyama hivyo vya upinzani vimeteleza wapi?

Kuhusu kuwa na sera nzuri, hakuna shaka kwamba vyama hivyo vina sera nzuri hata wakati mwingine viongozi wa Ukawa wamekuwa wakijigamba kuwa Serikali ya CCM imekuwa ikitekeleza baadhi ya sera za upinzani.

Katika uchaguzi mdogo wa udiwami uliofanyika Juni 16, 2013 CCM ilifanikiwa kushinda viti vya udiwani katika kata 16 huku Chadema ikiambulia viti sita vya udiwani kwenye kata 22.

Kwa matokeo hayo ni kama ishara kwa CCM kufanya vizuri zaidi katika uchaguzi wa kuchagua wenyeviti wa Serikali za Mitaa ifikapo mwaka 2019 na katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Kata ya Kiwanja cha Ndege

Uchaguzi mdogo uliomalizika Januari 22 Kata ya Kiwanja cha Ndege, Manispaaa ya Morogoro ilikuwa miongoni mwa kata 19 zilizoingia kwenye mbio za kumpata diwani kufuatia diwani aliyeingia madarakani katika Uchaguzi Mkuu 2015, Godfrey Nkondya kufariki dunia Machi, mwaka jana. Katika kampeni za uchaguzi huo uliingia dosari baada ya watu wanane kujeruhiwa na kulazimika kuwahishwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro kupata huduma ya kitabibu baada ya kutokea kwa vurugu. Kada wa Chadema, Martha Maeda (33) alijeruhiwa kwa kuchomwa mkuki katika mkono wa kulia na watu wasiojulikana baada ya kuvamiwa kambi yao iliyokuwa Mtaa wa Kimunyu majira ya saa 10 alfajili wakati akiandaa chai Januari 15 mwaka huu.

Tukio lingine ni lile la Mwanahamisi Saidi (34) kujeruhiwa juu ya jicho la kushoto kwa kupigwa na kitu kilichodhaniwa kuwa ni jiwe baada ya kutokea vurugu kati ya wafuasi wa CUF na Chadema katika Mtaa wa Kimunyu saa tano asubuhi Januari 21.

Wengine waliojeruhiwa ni makada wa CCM, Iddy Juma, Lukoo Chingwi na Gerald Jeilan baada ya kutokea vurugu kati yao na wafuasi wa Chadema. Wanachama wanaodaiwa kuwa wa CUF waliojeruhiwa ni Ester Apian, Mariam Kiswila na Said Mussa.

Matukio hayo ya makada kujeruhiwa yalitokana na mwingiliano kati ya wafuasi wa vyama hivyo kwa kukutana ana kwa ana au ngome zao kuvamiwa na wenzao hali iliyozalisha ugomvi na vurugu na kusababisha kutumika kwa nguvu hasa silaha za jadi.

Baada ya wananchi kupiga kura Januari 22 mgombea wa CCM, Isihaka Sengo aliibuka mshindi kwa kupata kura 1,424 huku Salum Milindi wa Chadema akishika nafasi ya pili kwa kura 1,232 wakati CUF kupitia mgombea wake, Abeid Mlapakolo alipata kura 331.

Vyama vingine vilivyopata kura ni ACT-Wazalando (13), SAU (nne) na TLP haikupata kura hata moja.

Mtazamo wa wananchi

Mkazi wa Mtaa wa Kazongwa Kiwanja cha Ndege, Zawadi Juma (40) anaeleza kuwa matokeo ya uchaguzi yamekuwa ya kushangaza tofauti na baadhi ya wananchi walivyodhani Chadema ingeweza kupata kiti cha udiwani kutokana na kujaza watu katika kampeni zao. “Chadema nafikiri wanapaswa kujiuliza mazingira ya kukosa udiwani kata hii dhidi ya wenzao wa CCM walioshinda,” anasema.

Zawadi anasema kilichowaangusha Chadema ni kushindwa kujenga umoja wao wa Ukawa. Pia, kuibuka kwa vurugu katika baadhi ya mikutano ya kampeni.

“Ukawa wangejenga nguvu na umoja, mgombea wao angeshinda uchaguzi maana kuna kura zilizoenda kwa CUF na TLP, hizo zote zilikuwa mali yao na naiona sababu kubwa inatokana na mgogoro uliopo katika umoja huo,” anasema Zawadi.

Mgombea wa CUF

Aliyekuwa mgombea udiwani kupitia CUF, Abeid Mlapakolo anasema kushindwa kwake katika uchaguzi huo aliopata kura 331 kumetokana na chama hicho kuzidiwa mbinu na CCM na Chadema.

“Uchaguzi huu ulikuwa na ushindani mkali na kushindwa kwa  CUF kumechangiwa na mambo mengi, tulizidiwa mbinu dakika za mwisho kwa maana siku moja kabla ya kupiga kura na siku yenyewe ya kupiga kura baadhi ya wananchi walirubuniwa kwa kupewa fedha ili wakipigie kura chama fulani,” anasema Mlapakolo.

Mlapakolo anaeleza kuwa tayari amempongeza mgombea wa CCM, Sengo kwa kushinda udiwani, lakini akamtaka kutekeleza ahadi zote ili kata hiyo iendelee kimaendeleo.

“Kata ya Kiwanja cha Ndege ipo nyuma kimaendeleo katika Manispaa licha ya kuwa kongwe, hivyo diwani aelekeze ahadi zake za kwenye kampeni na anapaswa kusimama kidete katika vikao vya baraza la madiwani kuomba miradi ya maendeleo,” anasema.

Mgombea wa Chadema

Aliyekuwa mgombea udiwani kupitia Chadema, Salum Milindi anasema wapigakura walitishwa na Polisi kutokana na ulinzi mkali uliokuwapo. “Uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka 2015 watu zaidi ya 9,000 walijitokeza kupiga kura, lakini uchaguzi huu mdogo hawakuzidi watu 3,500,” anasema Milindi.

Anasema idadi kubwa ya wananchi kushindwa kujitokeza kupiga kura imeharibu ndoto zake za kuwatumikia wananchi wa Kiwanja cha Ndege kupitia nafasi ya udiwani, lakini bado hajakata tamaa na atahakikisha vipaumbele vyake vyote anavitetea kupitia kwenye baraza la maendeleo la kata akiwa mwenyekiti wa Serikali ya mtaa.

Anaongeza kuwa kilio chake kikubwa ni kuona jengo la zahanati linasimamiwa vyema na kukamilika.

Pia, mwanasiasa huyo analilia miundombinu kufanyiwa matengenezo kwa kuwekewa mifereji pembeni mwa barabara ili maji yasiharibu barabara itumike kipindi chote cha masika na kiangazi tofauti na sasa.

“Ni aibu baadhi ya barabara haziwezi kupitika hata kiangazi kutokana na ubovu. Kwa upande wa zahanati Januari hii ilitakiwa iwe kwenye hatua ya kupaka rangi na kuanza kuhudumia wananchi ndiyo maana kila mgombea amekuwa akizisemea kero hizo katika mikutano ya kampeni,” anasema Milindi.

Mgombea wa CCM

Sengo ambaye aliibuka kidedea katika uchaguzi huo mdogo, anawashukuru wananchi kwa kumchagua, lakini kazi iliyopo mbele yake ni kuhakikisha miradi yote ya Serikali iliyokwama inamaliziwa.

“Kazi yangu ya kwanza ni kuhakiki miradi yote ya Serikali iliyokwama ili nijue wapi pa kuanzia, lakini suala la uzoaji taka ngumu majumbani hilo limekuwa katika kipaumbe cha pili kisha nitatembelea Soko la Mawenzi kuangalia namna ya kuondoa au kupunguza changamoto za uchafu,” anasema mwanasiasa huyo.

Anasema wananchi wa kata hiyo amewaomba kuungana na kuwa kitu kimoja ili kuijenga Kiwanja cha Ndege kwani anaamini kwamba maendeleo hayawezi kuletwa na mtu mmoja.

Katika uchaguzi huo mdogo CCM imekuwa ikishutumiwa kushinda kutokana na kutumia nguvu nyingi za rasilimali watu kutoka vyombo vya dola.

Mkurugenzi wa Uchaguzi Jimbo la Morogoro Mjini, John Mgalula anaeleza kuwa kulikuwa na vituo 25 vya kupigia kura ambavyo vilitumika katika mitaa 13 ya kata hiyo wakati jumla ya wapigakura walio halali ni 10,444 waliotarajiwa kupiga kura kwa wagombea wa vyama sita vilivyoingia katika kinyang’anyiro hicho.

Anataja vyama vilivyoshiriki uchaguzi huo kuwa ni Chadema, CCM, CUF, ACT-Wazalendo, TLP na Sau na kueleza kuwa wananchi walijitokeza kupiga kura kwa amani na utulivu.

Usumbufu kwa waandishi

Mkurugenzi huyo wa uchaguzi alilazimika kuwaomba radhi waandishi wa vyombo vya habari kutokana na changamoto kutoka kwa wasimamizi wa vituo baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jimbo la Morogoro kushindwa kuandaa vitambulisho kwa ajili yao. 

Waandishi hao waliombwa radhi baada ya kukutana na majibu yasiyo na staha kutoka kwa wakuu wa vituo vya kupigia kura na pale walipojitambulisha kwa vitambulisho vya kampuni zao ilikuwa vigumu kueleweka kwa mabosi hao.

Hali hiyo ilimlazimu msimamizi wa uchaguzi huo kuandika barua za utambulisho na kuwakabidhi waandishi wa habari majira ya saa nne asubuhi baada ya malalamiko.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ferdinand Leonce anaeleza kuwa katika uchaguzi huo zipo taarifa zilizoripotiwa katika jeshi hilo na kwamba watu wanne wamefikishwa mahakamani kwa kuvunja sheria na taratibu za nchi.

“Tumepokea taarifa za watu kujeruhiwa na baadhi yao walipata michubuko, lakini walilazimika kulazwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro na sasa wameruhisiwa kuendelea na shughuli zao,” anasema Leonce.