Mambo 15 ya kufanya kupata hati mpya ya kusafiria

Muktasari:

Maelekezo hayo yametolewa na Idara ya Uhamiaji

Dar es Salaam. Siku 10  baada ya Rais John Magufuli kuzindua hati ya kielektroniki ya kusafiria, Idara ya Uhamiaji imetoa maelekezo ya  kujaza fomu za maombi kwa njia ya mtandao.

Msemaji wa Uhamiaji, Ally Mtanda amesema leo Februari 9, 2018 kuwa fomu hizo zipo kwa Kiswahili na kusisitiza kuwa mwombaji anapaswa kuwa na kitambulisho cha Taifa ili kukidhi moja ya sharti muhimu.

“Maombi kwa sasa ni mengi, changamoto ni baadhi ya waombaji kutokuwa na vitambulisho vya Taifa ambavyo sasa wanaona umuhimu wake na kulazimika kuvifuata Nida (Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa),” amesema Mtanda.

Pia, amesema muda ambao utatumika hadi mwombaji kupata hati yake ya kusafiria ni chini ya siku 14 za kazi ingawa hakubainisha ni siku ngapi.

Amesema mwombaji anayehitaji kupata hati hiyo, kwanza anapaswa kuingia  katika tovuti ya Idara ya Uhamiaji www.immigration.go.tz na kisha kwenda katika kitufe cha e-Services.

Pili, mwombaji atapaswa kuchagua fomu ya maombi ya hati. Tatu, kuchagua ombi jipya, nne, atatakiwa kutiki kiboksi kukubaliana na maelekezo na tano anaanza kujaza taarifa zake kwa ukamilifu ukifuata maelekezo na mpangilio katika kila kipengele.

Baada ya mwombaji kukamilisha kujaza taarifa zake, atafahamishwa ya kwamba usajili umekamilika na kupatiwa namba ya ombi, ambayo ni muhimu aiandike pembeni na kuihifadhi kwa kumbukumbu za baadae.

Amesema mwombaji atapewa namba ya kumbukumbu ya malipo na kutakiwa kwenda kulipia malipo ya awali  Sh20,000.

Mtanda amesema baada ya mwombaji kumaliza hatua hiyo, ukurasa huo, ataingia katika menu ya M-Pesa/Tigopesa (*150*00#/*150*01#).

Amesema baada ya hapo atatakiwa kubonyeza namba 4 (lipa kwa M-Pesa) au kubonyeza namba 4 (kulipia bili)-Tigo na baada ya kuchagua mtandao wa malipo, atatakiwa kuingiza namba ya kampuni 888999.

Mwombaji pia atatakiwa kuingiza kumbukumbu namba (Ingiza Control Number inayoanzia na 99109…….), kisha kiasi (kama ilivyo elekezwa Mfano: 20,000), atapata  maelezo kuwa unalipa pesa NMB, baada ya hapo ataingiza namba ya siri, atahakiki na kupata ujumbe mfupi wa maneno kutoka M-Pesa/Tigopesa kama muamala umekubalika.

Amesema baada ya hatua hiyo mwombaji atapata ujumbe  kutoka kwenye mfumo namba 15200 kama muamala umekubalika, kisha kurudi  katika ombi linaloendelea na mwisho ataingiza namba ya ombi au simu na namba ya risiti na hapo atapakua fomu yake ya maombi.

Mtanda amesema baada ya kuwa amepata fomu atatakiwa kuiwasilisha katika Ofisi ya Uhamiaji makao makuu au Ofisi Kuu Zanzibar.

Amesema malipo hayo yanaweza kufanyika pia kwa njia ya benki NMB/CRDB ambapo mwombaji atapaswa kujaza fomu ya malipo ya kielectroniki, kufuata maelekezo kama yanavyojieleza kwenye fomu, atapata meseji kutoka benki na kwenye mfumo namba 15200 kama muamala umekubalika.