Ukuta mikononi mwa Magufuli

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (kulia) akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya chama hicho, Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis

Muktasari:

Hata hivyo, Chadema imesema uamuzi wao wa kuahirisha maandamano na mikutano hautokani na vitendo vya kukamatwa kwa viongozi wa chama hicho, Polisi kufanya mazoezi ya wazi hadharani, Jeshi la Wananchi (JWTZ) kutangaza Septemba Mosi kuwa siku ya usafi wakati ilishafanya Julai 25 na kauli za vitisho za viongozi wa Serikali.

Dar es Salaam. Chadema imetaja sababu tatu za kuahirisha kwa mwezi mmoja mpango wake wa kuandamana na kuendesha mikutano ya hadhara kote nchini kuanzia leo, kuwa ni kutoa nafasi kwa viongozi wakuu wa dini kuzungumza na Rais John Magufuli kutafuta suluhu ya kudumu ya madai yao.

Hata hivyo, Chadema imesema uamuzi wao wa kuahirisha maandamano na mikutano hautokani na vitendo vya kukamatwa kwa viongozi wa chama hicho, Polisi kufanya mazoezi ya wazi hadharani, Jeshi la Wananchi (JWTZ) kutangaza Septemba Mosi kuwa siku ya usafi wakati ilishafanya Julai 25 na kauli za vitisho za viongozi wa Serikali.

Uamuzi wa kuendesha mikutano na maandamano kote nchini ulifikiwa na Kamati Kuu ya Chadema iliyokutana kwa siku mbili jijini Dar es Salaam na kutangazwa Julai 27.

Jana, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwaambia waandishi wa habari kuwa baada ya viongozi kadhaa wa dini, mke wa Baba wa Taifa na taasisi nyingine kuongea na viongozi, chama hicho kimeamua kuahirisha uzinduzi wa harakati hizo kwa siku 30 ili wakuu hao waweze kuzungumza na Rais John Magufuli na Serikali yake.