Ukuta wa Chadema wamuibua Msajili

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari alipokuwa akitangaza maazimio ya kamati kuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam juzi. Picha na Venance Nestory

Muktasari:

Wakati CCM ikiwataka Watanzania kutafakari kabla ya kuamua kuungana na viongozi wa Chadema “kudai demokrasia” na kugeuka kafara kwa vyombo vya ulinzi na usalama, Jaji Mutungi amesema kauli za chama hicho cha upinzani ni kinyume cha Sheria ya Vyama vya Siasa.

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Chadema kutangaza mikakati mitatu ya kupinga ilichokiita ukandamizaji wa haki na demokrasia, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na CCM wameibuka wakikituhumu chama hicho kikuu cha upinzani nchini kutoa kauli wanazodai zimejaa uchochezi.

Wakati CCM ikiwataka Watanzania kutafakari kabla ya kuamua kuungana na viongozi wa Chadema “kudai demokrasia” na kugeuka kafara kwa vyombo vya ulinzi na usalama, Jaji Mutungi amesema kauli za chama hicho cha upinzani ni kinyume cha Sheria ya Vyama vya Siasa.

Lakini wakati Msajili na CCM wakisema hayo, wasomi waliohojiwa na Mwananchi wamesisitiza kauli iliyotolewa na mwenyekiti wa zamani wa CCM, Jakaya Kikwete kuwa chama bila kufanya shughuli za siasa kama mikutano ya hadhara, ni kazi bure na kwamba shughuli za siasa haziwezi kuathiri ukuaji wa uchumi.

Juzi mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema moja ya mikakati yao ni kufanya maandamano na mikutano nchi nzima kuanzia Septemba Mosi mwaka huu.

Alisema uamuzi huo, ambao ni moja ya maazimio ya Kamati Kuu unalenga kuashiria kupinga kauli ya Rais John Magufuli na Jeshi la Polisi kuzuia mikutano ya hadhara ya kisiasa.

Mbali na mkakati huo, Chadema imeanzisha operesheni iliyopewa jina la Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta), ikitaja matukio 11 inayodai kuwa ya ukandamizaji wa demokrasia nchini na mengine 24 yaliyosababisha kuzinduliwa operesheni Ukuta.

Kauli ya CCM

Lakini msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka aliwaambia waandishi wa habari jana kwenye ofisi ndogo za makao makuu ya CCM kuwa kauli zilizotolewa na Mbowe zimejaa upotoshaji na uongo uliokithiri, na kufafanua kuwa Serikali haijazuia mikutano ya hadhara kwenye majimbo na kwamba wapinzani wanatapatapa kutokana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano.

“Eti Serikali hii ni ya kidikteta? Udiketa upi unaosemwa? Je, ni huu wa kubana wakwepa kodi, kupunguza safari za nje, kubana matumizi ya Serikali, kufukuza wabadhirifu na wazembe kazini?” alihoji ole Sendeka huku akisema Watanzania wengi wanaunga mkono mambo yanayofanywa na Rais.

“Wamezoea kujenga chama chao kwa harakati zinazohusisha kumwaga damu za Watanzania wasio na hatia. Ukweli wa Serikali hawausemi isipokuwa wanafanya juhudi kubwa kuhakikisha wanafanya mambo ambayo yatasababisha vurugu, uvunjifu wa amani na umwagaji damu.”

Ole Sendeka alisema kama Chadema ina nia njema inapaswa kufuata sheria.

“Demokrasia bila mipaka ni fujo,” alisema.

Jaji Mutungi alonga

Wakati ole Sendeka akiwaambia hayo waandishi wa habari, Jaji Mutungi alituma taarifa yake kwenye vyombo vya habari akisema tamko la Chadema limejaa lugha za uchochezi, kashfa na kuhamasisha uvunjifu wa amani.

Mlezi huyo wa vyama vya siasa alisema kifungu cha 9(2)(f) kinakataza chama cha siasa kuruhusu viongozi au wanachama wake kutumia lugha ya matusi, kashfa na uchochezi ambayo inaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

“Kanuni ya 5(1)(d) inakitaka kila chama cha siasa kutotoa maneno yoyote au maandishi ambayo ni uongo kuhusu mtu yeyote au chama cha siasa. Tamko la Chadema ni ukiukwaji wa sheria na si mara ya kwanza chama hiki kutoa kauli hizi,” alisema Jaji Mutungi.

Jaji Mutungi alisema vyama vya siasa vinatakiwa kutimiza wajibu wake kwa weledi kama taasisi za kisiasa na kuonyesha ukomavu na kuepuka vitendo na kauli za uchochezi na kuvitaka kufuata njia sahihi za kidemokrasia za mawasiliano ya taasisi za umma kuwasilisha malalamiko au hoja mbalimbali.

 

Maoni ya wasomi

Baadhi ya wadau waliohojiwa na Mwananchi waliungana na harakati za Chadema.

“Naunga mkono jitihada za kuimarisha demokrasia. Katika hilo hakuna mtu atakayepinga kwa kweli ila kunaweza kuwa na njia tofauti za kudai kuimarishwa kwa demokrasia,” alisema Profesa Kitila Mkumbo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Profesa Kitila alisema anaungana na Chadema katika mkakati wake wa kuidai demokrasia ya kweli na si kupinga udikteta.

“Ninachokimaanisha ni kuilinda na kuipigania demokrasia sio kupambana na udikteta.”

Kauli ya Profesa Mkumbo iliungwa mkono na Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha ambaye pia aligusia uamuzi wa Jeshi la Polisi wa Julai 7 mwaka huu, kupiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya siasa kwa madai kuwa yana lengo la kuhamasisha wananchi kutotii sheria za nchi.

Jeshi la Polisi lilitoa tamko hilo baada ya kusambaratisha mkutano wa hadhara wa Chadema uliopangwa kufanyika Kahama, na baadaye kuzuia hafla ya ndani ya Chadema ya mahafali ya Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu kabla ya kuzuia mkutano wa ndani wa chama cha ACT Wazalendo wa kujadili bajeti ya mwaka 2016/17.

Uamuzi huo wa Jeshi la Polisi kuzuia shughuli hizo za kisiasa ulipigiwa msumari na Rais John Magufuli wakati akikabidhiwa ripoti ya Uchaguzi Mkuu, aliposema shughuli za siasa zinatakiwa zifanywe mwaka 2020 wakati wa Uchaguzi Mkuu na sasa ni wakati wa kazi, huku akieleza kuwa hangependa “mtu yeyote anicheleweshe kutekeleza ahadi zilizotoa kwa wananchi wakati wa uchaguzi”.

Lakini Profesa Mpangala alisema zuio hilo la Jeshi la Polisi si sahihi.

“Mfumo wetu Tanzania ni wa vyama vingi, huwezi kuvizuia kufanya shughuli za siasa. Sijui polisi watachukua hatua gani kwa Chadema. Niliwahi kusema hii kauli ya kuzuia mikutano ya hadhara itahatarisha amani ya nchi,” alisema Profesa Mpangala.

“Watu walizoea demokrasia, walizoea kufanya mikutano ya siasa. Kuwazuia si sahihi. Hili suala la kuzuia mikutano lilipaswa kuwa mjadala wa kitaifa. Ni uamuzi ambao haukupaswa kuchukuliwa.”

Richard Mbunda, mhadhiri wa UDSM alikwenda mbali zaidi kuzungumzia kauli ya Rais Magufuli akisema shughuli za siasa haziwezi kuathiri utekelezwaji wa ahadi za Serikali.

Pia alisema shughuli hizo za kisiasa haziwezi kuathiri ukuaji wa uchumi.

Wakili na mhadhiri wa UDSM, Dk James Jesse alisema: “Chama chochote cha siasa kikiona kinawekewa vikwazo, hakiwezi kukaa kimya maana wakifanya hivyo wataonekana wanafurahia wanachotendewa.”

Dk Jesse alisema walichokifanya Chadema kimetokana na imani yao kuwa haki inaminywa.

Akitoa mfano wa mawakili wa kujitegemea mkoani Arusha walioandamana kupinga mwenzao kukamatwa na polisi akiwa kazini, Dk Jesse alisema kitendo cha mawakili hao ndio demokrasia na kwamba hata mwenye makosa ana haki ya kusikilizwa.