Waziri aeleza mikakati kulinda rasilimali

Muktasari:

Ulega ameyasema hayo jana Machi 17, 2018 mkoani Kigoma mbele ya kamati hiyo ilipokuwa katika ziara ya kutembelea Chuo cha Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (Feta) kampasi ya mkoa huo.

 Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega ameileza Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuwa Serikali ina mpango wa kuifanya sekta ya mifugo na uvuvi iwe na mchango mkubwa kwenye pato la Taifa.

Ulega ameyasema hayo jana Machi 17, 2018 mkoani Kigoma mbele ya kamati hiyo ilipokuwa katika ziara ya kutembelea Chuo cha Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (Feta) kampasi ya mkoa huo.

Amesema wizara hiyo ina mikakati wa kulinda rasilimali za mifugo na uvuvi, kwa kuimarisha uvuvi wa bahari kuu na kuitoa sekta hiyo kwenye kuchangia kiasi na Sh19 bilioni kwa mwaka katika pato la Taifa hadi kufikia kuchangia zaidi ya Sh50 bilioni kwa mwaka.

“Tunaweza kufikia malengo haya kwa kuhakikisha taasisi yetu ya kusimamia uvuvi wa bahari kuu inakuwa na nguvu kwa kuweka vizuri sheria na kanuni zetu za uvuvi,”amesema Ulega.

Sambamba  na hilo, Ulega ameambia kamati hiyo kuwa  Serikali ina mkakati wa kuwa na meli ambayo itakuwa na uwezo wa kwenda kuvua na kuchakata mazao ya samaki, mpango utakaokwenda sambamba na ufunguaji wa viwanda vya uchakataji wa mazao ya uvuvi.

Katibu mkuu wa wizara hiyo anayesimamia sekta ya Uvuvi, Dk Yohana Budeba amesema njia ya ufugaji wa samaki wa kisasa kupitia ni kuwa, Feta itatengeneza wataalamu na kuongeza ajira sanjali na upatikanaji wa samaki wengi na kusababisha mchango mkubwa wa sekta ya uvuvi katika uchumi wa Taifa.