Tanesco yaeleza sababu za kukatika umeme

Muktasari:

Usafishaji na uungaji wa bomba kubwa la gesi katika Mitambo ya Kinyerezi I imetajwa kuwa chanzo cha kukatika umeme

Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema sababu ya kukatika umeme leo kuanzia saa mbili asubuhi ni usafishaji na uungaji wa bomba kubwa la gesi katika Mitambo ya Kinyerezi I, iliyopo jijini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na uongozi wa shirika hilo leo Jumamosi Novemba 18,2017 imesema sababu nyingine ni maandalizi ya uunganishaji wa Kituo cha Kinyerezi II.
Shirika hilo licha ya kuwaomba radhi wateja, limetoa taarifa kuwa huduma haitapatikana kuanzia pia kesho Jumapili Novemba 19,2017 kutokana na kazi hiyo.
“Kutokana na kazi hiyo kutakuwa na upungufu wa umeme katika Gridi ya Taifa, hivyo baadhi ya wateja waliounganishwa katika gridi wa maeneo mbalimbali nchini watakosa huduma ya umeme,’’  imesema taarifa hiyo.
Tanesco imesema, ‘’Zoezi hilo linaendelea kwa ufanisi mkubwa na haraka ili kurejesha huduma ya umeme kwa wakati.”
Shirika hilo limeahidi kutoa  taarifa zaidi za maendeleo ya kazi, huku likitoa tahadhari kwa wananchi wanaopita karibu na maeneo ya mitambo ya Kinyerezi kutokufanya shughuli za uchomeleaji vyuma na nyingine yoyote yenye viashiria vya moto ili kujikinga na madhara yanayoweza kutokea.