Mbeya Yaendelea kuwa gizani

Muktasari:

Amesema mafundi wanaendelea kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha kwamba huduma hiyo inarejea katika mkoa huo kama ilivyo kwenye mikoa mingine.

Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema huduma ya umeme imerejea saa 7.11 mchana nchi nzima isipokuwa mkoa wa Mbeya.

Huduma ya umeme ilikatika tangu jana katika mikoa yote iliyounganishwa katika gridi ya taifa.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa mchana, Desemba 1, 2017 na Kaimu Meneja Mawasiliano wa Tanesco, Leila Mhaji imesema mkoa wa Mbeya ndiyo pekee ambao huduma hiyo haijarejea kutokana na hitilafu iliyopo katika njia ya Mufindi.

Amesema mafundi wanaendelea kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha kwamba huduma hiyo inarejea katika mkoa huo kama ilivyo kwenye mikoa mingine.

“Tutaendelea kuwajulisha mara huduma hiyo itakaporudi kwani mafundi wanaendelea na kazi,” amesema. Amesema mapema leo huduma hiyo ilianza kurejea katika mikoa ya Iringa, Dodoma na Tanga

Amewaomba radhi wateja kwa usumbufu wowote uliojitokeza. Amesisitiza wananchi kutoshika wala kukanyaga waya uliokatika au kuanguka.