Unajua kuwa taasisi nazo zina siasa?

Muktasari:

Siasa za kitaasisi zinahusisha mbinu zisizo rasmi zinazotumiwa katika taasisi hasa na mameneja au viongozi katika kujiongezea ushawishi na nguvu katika taasisi kwa ajili ya kufikia matakwa binafsi na mara nyingine yale ya taasisi. Ifahamike kuwa japo siasa hizi hutumia mbinu zisizo rasmi lakini zikitumika vizuri huwa na manufaa kwa mustakabali wa taasisi husika. Kwa kuzingatia kuwa watu wengi huwa hawapendi au hawakubali mabadiliko kirahisi siasa hutumika katika kuwashawishi wafanyakazi kuyakubali mabadiliko hayo.

Kila ukisikia neno siasa inawezekana kabisa akili yako inafikiria moja kwa moja siasa za zinazofanywa na vyama vya siasa katika nchi yoyote. Ukweli ni kwamba siasa zimekuwa zikitumika sehemu mbali mbali; kwenye michezo, makanisani, majumbani lakini hata kwenye taasisi mbali mbali siasa imekuwa ikuchukua nafasi. Leo tunaangalia jinsi siasa za kitaasisi zinavofanya kazi kwenye mashirika na taasisi mbali mbali.

Siasa za kitaasisi zinahusisha mbinu zisizo rasmi zinazotumiwa katika taasisi hasa na mameneja au viongozi katika kujiongezea ushawishi na nguvu katika taasisi kwa ajili ya kufikia matakwa binafsi na mara nyingine yale ya taasisi. Ifahamike kuwa japo siasa hizi hutumia mbinu zisizo rasmi lakini zikitumika vizuri huwa na manufaa kwa mustakabali wa taasisi husika. Kwa kuzingatia kuwa watu wengi huwa hawapendi au hawakubali mabadiliko kirahisi siasa hutumika katika kuwashawishi wafanyakazi kuyakubali mabadiliko hayo.

Pamoja na hayo siasa hizi zinaweza kuwa kikwazo kwa ustawi wa taasisi. Pia viongozi na mabosi wasiojua kutumia siasa katika uendeshaji wa taasisi wako kwenye hatari ya kushindwa kumudu nafasi zao hivyo ni vyema kujua jinsi ya kukabiliana na siasa zinazoendeshwa na wafanyakazi wengine na jinsi ya kutumia siasa pia kulinda nafasi walizonazo na kusaidia taasisi kufikia malengo yake.

Muungano wa kimkakati. Mabosi wengi hutengeneza muungano wa kimkakati ili kuhakikisha wanalinda nafasi zao au wanahakikisha kuwa jambo fulani linafanikiwa au kupitishwa. Katika siasa za kichama hivi ni kama vyama vya siasa lakini mara nyingi watu wanaotengeneza muungano huu hawapendi kujulikana au kukubali kuwa muungano wao ni wakimkakati. Wakati mwingine ili bosi aendelee kuwa kwenye nafasi yake au kuongeza ushawishi huungana na baadhi ya watu ambao wao hutumika kumtetea na kutetea ajenda zake kwenye vikao na hata kwenye sehemu nyingine katika mazungumzo ya kawaida na wafanyakazi wengine.

Wanaokubali kuwa kwenye muungano huu uwa wanamatarajio fulani kutoka kwenye muungano huu. Nisaidie-nikusaidie uwa ndiyo utaratibu unaotumika hapa. Mabosi wengine uwaahidi wanachama wa ‘vyama’ vyao nafasi za uongozi, kuwalinda kwenye mambo mengine na wakati mwingine kuwapa fursa nyingine ambazo wengine hawatapata kirahisi.

Matumizi ya wataalam elekezi. Pale inapotokea jambo Fulani ni gumu kueleweka au kukubalika katika taasisi mtu kutoka nje ya taasisi hutumiwa ili kuongeza ushawishi. Hii ni njia yenye ufanisi mkubwa kwani wafanyakazi wanaposikia kuwa consultant kaelezea umuhimu wa sera fulani wanashawishika kirahisi kuliko mtu waliyemzoea katika taasisi au bosi wao wa kila siku.

Matumizi ya watoa taarifa. Mara nyingi katika kila taasisi viongozi hutengeneza mfumo usio rasmi wa kiintelejensia kwa kuwa na watu wanaowapa taarifa juu ya mambo yanayoendelea kwenye taasisi. Kwa kawaida siyo rahisi kwa wakuu katika taasisi kupata taarifa juu ya yanayosemwa au mpingo inayopangwa dhidi yao kutokana na kutokuwa karibu na vyanzo vya habari. Kukabiliana na hili viongozi hawa huwa na watu wanaowatumia katika kuwapa taarifa mbali mbali ili waweze kuandaa mikakati ya kujilinda na matishio yoyote dhidi ya nyadhifa zao, mipango na sera wanazozitekeleza au kutarajia kuzitekeleza.

Vitisho.

Hii ni njia iliyozoeleka mara ambayo viongozi na wabosi wengi huitumia kwa kutoa vitisho hadharani kwenye vikao au kuwaita watu wanaohisi wanachangia kuathiri mikakati yao na kuwatishia ili kuwafanya wakubali kuyafuata matakwa yao. Wakati mwingine viongozi hutumia hata njia zilizo rasmi kama kuwapa barua za onyo kwa kutumia sababu husika au hata kutunga sababu nyingine lakini mpokea barua huelewa kabisa nini chanzo cha onyo lile.

Kugawa na kutawala.

Pale viongozi wanaopoona kuna dalili za dhahiri kuwa hawaungwi mkono na wafuasi wanaungana kwa pamoja kuwapinga au kumpinga kiongozi, njia ambayo hutumika ni kuigawa taasisi hasa kisaikolojia ili iwe rahisi kuwatawala. Umeshawahi kuona idara zote zinaungana kuunga mkono jambo fulani lakini ghafla kiongozi anaanza kulisifia kundi (idara) moja na kuliacha jingine? Hii hupunguza nguvu ya umoja na kujikuta kundi moja likijiona liko upande wa kiongozi na jingine kuhisi aliko upande wake. Wakati mwingine ili kuhakikisha taasisi inagawanywa ili iweze kutawaliwa kirahisi mabosi au viongozi huchagua kwa makusudi kulipendelea kundi fulani kwa namna mbali mbali ikiwemo kulipa rasilimali nyingi zaidi ya jingine.

Matumizi ya taarifa za uongo au uzushi

Wapo viongozi au hata wafanyakazi ambao hutumia uzushi na uongo ili kuharibu sifa njema za wengine ili kuhakikisha wanafanikisha adhma fulani katika katika taasisi. Wapo wanaoamini kuwa utendaji mzuri wa kazi wa baadhi ya watu kwenye taasisi ni tishio kwenye nafasi zao hivyo kuamua kuzusha taarifa za uongo ambazo hutumia mfumo usio rasmi kuzisambaza. Sio kila maneno juu ya wengine kuwa ni wala rushwa, hawatendi haki, wabaguzi na mengineyo ni ya kweli bali ni siasa chafu ambazo hutumiwa na wengine katika kuwaharibia sifa njema.

Madhara ya siasa za kitaasisi

Siasa katika taasisi mbali mbali huwa ni kwa lengo la kutimiza matakwa binafsi ya viongozi na mara chache huwa kwa maslahi ya taasisi. Hii husababisha kupunguza ushirikiano na umoja katika taasisi kwani wengi huamini kuwa hawanufaiki na siasa hizo. Hii husababisha kuondoa hali na amasa ya kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo ya taasisi husika.

Ushindani usio na tija kwenye taasisi pia huibuka kwani tabaka lisilonufaika na siasa hizo mara nyingi uwa halikubali kushindwa kirahisi. Hii hufanya tabaka hilo kupinga karibu kila kitu kinacholetwa au kupendekezwa na viongozi hata kama mambo hayo yanatija kwa taasisi nzima.

Ili kuhakikisha siasa zinatumika vyema katika taasisi ni bora kuangalia ni jinsi gani zinachangia katika mustakabali wa taasisi husika ili kusaidia taasisi kufikia malengo yake. Kuangalia matakwa binafsi pekee ni kupoteza dira ya taasisi husika na kuigawa taasisi kitu kinachoua umoja na ushirikiano katika taasisi.

Kelvin Mwita ni Mhadhiri Msaidizi Chuo Kikuu Mzumbe na mtaalam wa rasilimali watu, 0659081838, [email protected], www.kelvinmwita.com