Unataka Sh1 bilioni? Mlete Mo Dewji

Azim Dewji ambae ni msemaji wa familia ya mfanyabiashara maarufu Mohammed Dewji akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara huyo. Kushoto ni baba wa Mohammed, aitwae Gulam. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Familia ya mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo’ na Kampuni Tanzu za Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL) leo  Jumatatu imezungumza na waandishi wa habari kuhusu kutekwa kwa bilionea huyo na kutangaza dau la Sh 1 bilioni kwa yeyote atakayefanikisha kumpata

Dar es Salaam. Familia ya mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo’ imetangaza dau la Sh1 bilioni kwa mtu yeyote atakayewezesha kupatikana kwa bilionea huyo kijana.

Akisoma taarifa ya familia mbele ya waandishi wa habari leo Jumatatu jijini Dar es Salaam, Azim Dewji amesema, “Yeyote atakayewezesha kupatikana kwa mtoto wetu mpendwa Mohammed atazawadiwa Sh1 bilioni.”

Azim, ambaye amejitambulikuwa kuwa ni mwanafamilia amesema yeyote atakayetoa taarifa zitakuwa za siri huku akiwaomba Watanzania kuendelea kuwaombea familia hiyo na mtoto wao apatikane akiwa salama.

Licha ya kujitambulisha kama mwanafamilia, Azim amewahi kuwa mfadhili wa klabu ya Simba mwanzoni mwa miaka ya 1990 na aliiwezesha timu hiyo kufika fainali ya Kombe la CAF kabla ya kutolewa na Stella Abdijan kwa mabao 2-0.

Katika mkutano huo wa leo Jumatatu uliohudhuriwa na vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi, baba mzazi wa ‘Mo’,  Gullam Hussein alikuwa amekaa pembeni mwa Azim wakati akisoma taarifa hiyo ya familia.

Azim alisema yeyote mwenye taarifa anaweza kuwasiliana nao kwa namba 0755030014 au 0717208478 na 0784783228.

Mo anayekadiriwa kuwa na utajiri wa Sh3.5 trilioni alitekwa Alhamisi iliyopita katika Hoteli ya Collosseum jijini Dar es Salaam alipokwenda kufanya mazoezi saa 11 alfajiri.

Mo ni mwekezaji wa klabu ya Simba na alikuwa katika mchakato wa kuwekeza Sh20 bilioni ili amiliki hisa 49 za klabu hiyo ya Msimbazi.