Unicef yawaokoa Watoto 145 vitani

Muktasari:

Mwakilishi wa Unicef Sudan Kusini, Mahimbo Mdoe amenukuliwa na vyombo vya habari akisema watoto hao walikuwa wanatumiwa na makundi yenye silaha ya la Riek Machar, mkuu wa waasi wa nchi hiyo na la Cobra katika mji wa Pibor wameokolewa.

Juba, Sudan Kusini. Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef) umesema zaidi ya watoto wadogo 145 waliokuwa wanatumika vitani nchini Sudan Kusini wameokolewa.

Mwakilishi wa Unicef Sudan Kusini, Mahimbo Mdoe amenukuliwa na vyombo vya habari akisema watoto hao walikuwa wanatumiwa na makundi yenye silaha ya la Riek Machar, mkuu wa waasi wa nchi hiyo na la Cobra katika mji wa Pibor wameokolewa.

Cobra ni kundi la waasi lililowahi kutiliana saini makubaliano ya amani na Serikali ya Sudan Kusini mwaka 2014.

Mwakilishi huyo alisema watoto hao wamenyang’anywa silaha na baada ya kufanyiwa uchunguzi wa afya na kuandikishwa majina yao katika mpango maalumu wa shirika hilo na kwamba watapewa nguo za kiraia.

Baada ya hapo watarudishwa kwa familia zao na kuendelea kupewa msaada wa chakula kwa muda wa miezi mitatu.

Alisema shirika hilo litaendelea na mpango wake wa kukomboa watoto zaidi wanaotumika vitani. Kwa mujibu wa shirika hilo, kuna watoto wadogo 16,000 wanaotumika vitani Sudan Kusini.

Mdoe alisema lengo lingine la Unicef ni kuhakikisha watoto hao wanarudi shuleni na kuandaliwa kuwa watumishi wazuri wa jamii zao kwenye umri wa ukubwani.

“Tunataka watoto hao walelewe katika makuzi bora,” alisema.