Uokoaji waliofariki dunia MV Nyerere kumalizika leo

Muktasari:

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Issack Kamwelwe amesema uokoaji wa miili ya waliofariki dunia baada ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere utakamilika leo Septemba 21, 2018 kabla ya saa 12 jioni

Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Issack Kamwelwe amesema uokoaji wa miili ya waliofariki dunia baada ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere utakamilika leo Septemba 21, 2018 kabla ya saa 12 jioni.

Amesema hata majeneza kwa ajili ya mazishi ya waliofariki dunia yameshaandaliwa na yapo tayari.

Kamwelwe ametoa kauli hiyo leo mchana wakati akihojiwa na kituo cha Utangazaji cha Taifa (TBC), akiwa eneo la tukio Kisiwa cha Ukara wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza.

Amesema uwepo wa majeneza hayo unaashiria kuwa shughuli ya mazishi itafanyika kadri itakavyowezekana.

“Hapa leo hatulali maana nimekuja na timu nzima jeshi lipo hapa, polisi wapo hapa na masanduku pia,”amesema.

“Shughuli za mazishi zitafanywa kwa kufuata taratibu zote ikiwemo kuzingatia mila na desturi na kwa kuzingatia taratibu za kidini kwa vile viongozi wote wa dini wapo.”

Alipoulizwa kuhusu sababu za kuzama kwa kivuko hicho, Kamwelwe amesema hawezi kulielezea jambo hilo kwa maelezo kuwa jambo hilo litafahamika baadaye.