Upanuzi barabara ya Mandela wakwamisha Tanesco

Naibu Katibu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dk Juliana Pallangyo

Muktasari:

Mradi huo, unatajwa kuwa ndiyo suluhisho la kukatika kwa umeme Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Mradi wa ujenzi wa barabara ya njia sita ikiwamo ya mwendo kasi kutoka Ubungo hadi bandarini, unatajwa kuwa chanzo cha kushindwa kukamilika kwa wakati mradi mkubwa wa usafirishaji wa umeme jijini hapa.

Mradi huo, unatajwa kuwa ndiyo suluhisho la kukatika kwa umeme Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kukutana na uongozi wa Wakala wa wa Barabara Tanzania (Tanroad) Mkoa wa Dar es Salaam juzi, Naibu Katibu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dk Juliana Pallangyo alisema mradi huo umetekelezwa kwa asimilia 86, lakini kwa sasa umekwama kutokana na ujenzi huo.

Mradi huo ulipangwa kukamilika Juni 30, nguzo za kusafirisha umeme huo ziliwekwa eneo ambalo barabara hizo zitapita.

Mkuu wa Idara ya Mipango wa Tanroad Dar es Salaam, Mhandisi Humphrey Kanyenye alisema awali walikubaliana na Tanesco waweke nguzo pembezoni mwa barabara, lakini walipopewa mradi wa barabara hiyo kubwa walijikuta wanahitaji eneo kubwa zaidi na kuingiliama na wa Tanesco.

“Hizo barabara ni kubwa, hivyo eneo lililopo sasa tunahitaji kuongeza mita 10 kila upande, lakini hatujazuia eneo kwa nia mbaya, huo mradi tunautambua umuhimu wake naamini tutapata suluhisho,” alisema Kanyenye.

Meneja Mwandamizi wa mradi wa Tanesco, Mhandisi Gregory Chegere alisema ni mradi muhimu kutokana na mahitaji makubwa ya nishati hiyo jijini hapa.