Upelelezi kesi vigogo TPDC haujakamilika

Muktasari:

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni  12, 2018

Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya matumizi mabaya ya madaraka inayowakabili vigogo watano wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu bado haujakamilika.

Wakili wa Takukuru,Maxi Ali  alieleza hayo  leo Jumatano Mei 23, 2018  mbele ya Hakimu Mkazi, Martha Mpazi wakati kesi hiyo ilipopangwa kwa ajili ya kutajwa ili  kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

Ali amedai mahakamani hapo kuwa  kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi wake bado haujakamilika, kuomba   ipangiwe tarehe nyingine ya kutajwa. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni  12, 2018.

Washtakiwa wanaokabiliwa na kesi hiyo ni aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, James Mataragio; Kaimu Meneja wa uvumbuzi, George Seni;  Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na utawala, Wellington Hudson;  Mkurugenzi wa Mkondo wa juu, Kelvin Komba na Edwin Riwa ambaye ni kaimu Mkurugenzi wa mipango.

Kwa  pamoja wanadaiwa kuwa kati ya Aprili 8,2015 na Juni 3,2016  wakiwa watumishi wa umma na waajiriwa wa TPDC kwa nafasi zao, wakati wakitimiza majukumu yao kwa makusudi walitumia madaka  vibaya.

Wanadaiwa kubadilisha na kupitisha bajeti na mpango wa mwaka wa manunuzi wa mwaka 2014/15 na 2015/16 kwa kuingiza ununuzi wa kifaa cha utafiti cha airborne gravity gradiometer survey ndani ya Ziwa Tanganyika  bila ya kupata kibali cha bodi  ya wakurugenzi ya shirika.

Amedai kuwa kitendo  hicho kinakiuka kifungu cha 49(2) cha Sheria ya manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 kwa lengo la kujipatia manufaa yasiyohalali ya dola 3,238,986.50 za Marekani ambazo ni takribani Sh7.2 bilioni kwa Bell Geospace.

Baada ya kusomewa shtaka hilo, washtakiwa wote walikana na  wapo nje kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kila mshtakiwa kuwa  na wadhamini wawili ambao walisaini bondi ya Sh 1 bilioni.