Upelelezi kesi ya mhasibu ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji haujakamilika

Muktasari:

  • Upande wa mashtaka katika kesi ya utakatishaji na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu inayomkabili mhasibu wa ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji,  Joyce Mushi (56) umeieleza Mahakama kutokamilika kwa upelelezi wa shauri hilo

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya utakatishaji na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu inayomkabili mhasibu wa ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji,  Joyce Mushi (56) umeieleza mahakama kutokamilika kwa upelelezi wa shauri hilo.

Mushi  mkazi wa Temeke, anakabiliwa na mashtaka ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi, wizi na utakatishaji wa fedha akiwa mtumishi wa umma katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakili wa Serikali, Nalindwa Sekimanga  amedai leo Jumanne Oktoba 9, 2018 mbele ya hakimu mkazi mkuu wa mahakama hiyo, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo iliyokuja kwa ajili ya kutajwa.

"Mshtakiwa yupo  mbele ya mahakama yako, kesi hii ilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," amedai Sekimanga.

Baada ya maelezo hayo wakili wa utetezi, Nehemia Nkoko  aliuomba upande wa mashtaka ujitahidi kukamilisha upelelezi kwa wakati, kwa sababu mteja wake yupo ndani na hana dhamana.

Hakimu Shahidi ameahirisha  kesi hiyo hadi Oktoba 23, 2018.

Katika kesi hiyo ya jinai namba  340/2017,  Joyce anadaiwa kuwa  Oktoba 25, 2016 katika ofisi za ubalozi wa Tanzania zilizopo Maputo nchini Msumbiji, alighushi barua na akijaribu kuonyesha kuwa ofisi ya ubalozi umeilekeza Benki ya Millennium (BIM) ya Maputo kuhamisha Dola 10,000 za Marekani kutoka kwenye akaunti namba 79667362 kwenda akaunti namba 182283177 inayomilikiwa na Mushi.

Inadaiwa kuwa akaunti zote hizo  zipo katika benki hiyo iliyopo tawi la Julius Nyerere, mjini Maputo.

Mshtakiwa anadaiwa Februari 10, 2017 katika ofisi za ubalozi huo, alighushi barua kuonyesha ubalozi umeielekeza benki hiyo kuhamisha Dola 10,000 kutoka akaunti namba 79667362 kwenda akaunti namba 182283177 inayomilikiwa na Mushi.

Pia, Aprili 12, 2017 katika ofisi za ubalozi huo alighushi barua akijaribu kuonyesha kwamba ubalozi umeielekeza BIM  kuhamisha Dola 40,000 kutoka akaunti namba 79667362 kwenda 182283177.

Oktoba 25, 2016 mshitakiwa katika benki hiyo tawi la Julius Nyerere, Maputo nchini Msumbiji anadaiwa aliwasilisha nyaraka za kughushi ambayo ni barua ya Oktoba 25, 2016 akionyesha kuwa ubalozi wa Tanzania nchini humo umeelekeza benki hiyo kuhamisha Dola 10,000 kutoka kwenye akaunti ya benki hiyo kwenda kwenye akaunti inayomilikiwa na mshitakiwa.

Pia,  imedaiwa  Oktoba 25, 2016 na Aprili 12, 2017 akiwa mtumishi  wa umma kama mhasibu wa ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji, aliiba Dola 150,000 mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.