Upelelezi kesi ya mke wa Bilionea Msuya wakamilika

Muktasari:

  • Mahakama ya Kisutu, Novemba Mosi, 2018 itawasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo, mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita na mfanyabiashara Revocatus Muyella wanaodaiwa kumuua dada wa bilionea Msuya

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Novemba Mosi, 2018 kuwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo, mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita na mfanyabiashara Revocatus Muyella wanaokabiliwa na shtaka la mauaji.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu Oktoba  22, 2018 na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo,  Thomas Simba baada ya upande wa mashtaka kuieleza mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika.

"Kwa kuwa upelelezi wa kesi hii umekamilika mahakama hii itawasomea maelezo ya mashahidi Novemba Mosi mwaka huu,” amesema Hakimu Simba.

Mrita na Muyella wanakabiliwa na shtaka moja la mauaji wakidaiwa kumuua kwa makusudi Aneth Msuya,  dada wa marehemu bilionea Erasto Msuya.

Awali, wakili wa Serikali mwandamizi, Patrick Mwita amedai kuwa upelelezi wa shauri hilo umeshakamilika na kuwaombea tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo.

"Upelelezi wa shauri hili umeshakamilika na jalada tayari limeshatoka kwa DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka) na sasa tunalo hapa. Hivyo tunaomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo,” amedai Mwita.

Baada ya kueleza hayo, wakili wa utetezi, Peter Kibatala alikubaliana na upande wa mashtaka na kuiomba mahakama ipange tarehe ya karibu ili wateja wake waweze kusomewa maelezo hayo.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza hoja za pande zote ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba Mosi, 2018.

Siku hiyo upande wa mashtaka utawasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo vilivyopo katika kesi hiyo kabla ya kuanza kusikilizwa ushahidi Mahakama Kuu.

Katika kesi hiyo ya mauaji namba 5 ya mwaka 2017, washtakiwa hao wanadaiwa kumuua kwa makusudi Aneth Msuya.

Tukio hilo, linadaiwa kufanywa Mei 25, 2016 maeneo ya Kibada Kigamboni, Dar es Salaam. Washtakiwa hao, awali Februari 23, 2016, waliachiwa huru katika kesi ya mauaji namba 32 ya mwaka 2016 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mwambapa.

Baada ya kufutwa kwa kesi hiyo iliyokuwa ikifanana na hii baadaye walikamatwa  na kusomewa upya mashitaka ya mauaji.