Upelelezi kesi ya ugaidi waibua tishio la mgomo

Muktasari:

Wanadai wamechoka kwenda mahakamani kuambiwa upelelezi haujakamilika

Arusha. Washtakiwa wa matukio ya ugaidi ikiwamo urushwaji wa mabomu katika maeneo mbalimbali mkoani Arusha wametangaza mgomo wa kuhudhuria mahakamani ili kushinikiza kukamilishwa upelelezi wa kesi dhidi yao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Nestory Baro washtakiwa hao walidai wamekuwa wakizungushwa kutokana na mashauri dhidi yao kutokamilika hivyo kukaa muda mrefu mahabusu bila kesi ya msingi kusikilizwa.

Washtakiwa hao 61 wanaokabiliwa na mashtaka tofauti katika kesi 15, walidai wamekuwa wakiambiwa upelelezi haujakamilika, lakini wanaamini kinachofanyika ni kunyimwa haki zao za kikatiba.

“Ni mwaka wa nne sasa tangu tukamatwe na kesi tuliyopewa ni ya ugaidi, lakini tumekuwa tukizungushwa; tunakwenda, tunarudi na wimbo ni uleule wa upelelezi haujakamilika. Tumechoka kuzungushwa,” alidai mmoja wa washtakiwa mahakamani hapo.

Mwingine alidai: “Tumetengana na familia zetu, haziruhusiwi kutuona, mpaka sasa kesi ya msingi haijaanzwa kusikilizwa. Tunaitaka Serikali ituite pale itakapokuwa imekamilisha upelelezi na kama hawatakamilisha waamue, watoe taarifa kuwa tuko kizuizini kwa muda usiojulikana ili tukae mahabusu milele au tufe. Tunataka upelelezi ukamilike haraka kesi ya msingi ianze lakini familia zetu ziruhusiwe kuja kutuona.”

“Tunatolewa kwa vitisho mji mzima unasimama tukipitishwa sisi, tunakuja tunapigishwa magoti, tunanyanyaswa watu wanaona na wanajua yanayotendeka lakini wameamua kukaa kimya,” alilalamika mshtakiwa mwingine.

Mshtakiwa mwingine alimuomba Rais John Magufuli kuingilia kati mwenendo wa kesi hiyo kwa kuwa inampotezea matumaini ya ndoto zake za kusoma.

Baada ya kusikiliza malalamiko yao, Hakimu Baro alisema atawasiliana na mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Mkoa wa Arusha kuhusu tamko lao la kutohudhuria mahakamani.

Alisema mkuu huyo wa upelelezi aliwapa miezi miwili kusikiliza malalamiko yao, hivyo atampigia simu kujua alipofikia.

Hakimu Baro alisema ni lazima wafike mahakamani Aprili 11 kesi itakapotajwa.