Upelelezi wakamilika kesi ya kina Kubenea

Muktasari:

Kubenea ambaye ni Mbunge wa Ubungo aliunganishwa kwenye kesi hiyo na  kuwa mshtakiwa wa sita. Mdee na Waitara pia ni wabunge wa Kawe na Ukonga.

Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya kumjeruhi Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresa Mmbando inayowakabili Saed Kubenea, Halima Mdee, Mwita  Waitara na wengine watatu, umekamilika.

Wakili wa Serikali, Flora Massawe mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ameiomba Mahakama ipange tarehe kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Baada ya ombi hilo, Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 12, washtakiwa watakaposomewa maelezo hayo kuhusu shtaka linalowakabili.

Kubenea ambaye ni Mbunge wa Ubungo aliunganishwa kwenye kesi hiyo na  kuwa mshtakiwa wa sita. Mdee na Waitara pia ni wabunge wa Kawe na Ukonga.

Washtakiwa  wengine ni Manase Njema, ambaye pia ni diwani wa Kimanga,  mfanyabiashara Rafii Juma na Ephraim Kinyafu, ambaye ni diwani wa Saranga Kimara.

Wanadaiwa Februari 27,  katika Ukumbi wa Karimjee, wilayani Ilala Dar es Salaam walimjeruhi Theresia na kumsababishia majeraha. Washtakiwa wapo nje kwa dhamana