Upepelezi kesi ya raia wa Marekani haujakamilika

Muktasari:

Mshtakiwa alikutwa akisafirisha dawa ya kulevya aina ya heroine yenye uzito wa kilo 2,188

Dar Es Salaam. Upande wa mashtaka  katika kesi ya kusafirisha dawa za kulevya inayomkabili raia  wa Marekani mkazi wa jimbo la Michigan, Lione Rayford (65) umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

 

Hayo yameelezwa na wakili wa Serikali Erick Shija leo Julai 20, 2018  mbele ya Hakimu Mkazi mwandamizi, Wanjah Hamza, kueleza kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa.

 

"Kesi hii imekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wa shauri hili bado haujakamilika" amedai Shija.

 

Baada ya maelezo hayo, hakimu Hamza aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti Mosi, 2018 kwa ajili ya kutajwa.

 

Katika mashtaka yake, Rayford anadaiwa kusafirisha  dawa za kulevya kinyume na kifungu cha sheria namba 15 (1) (a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na dawa za kulevya ya mwaka 2017.

Shija amedai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Julai 4,  2018 katika  Uwanja wa Ndege wa Kimataifa ya Julius Nyerere (JNIA).

 

Amedai mshtakiwa alikutwa akisafirisha dawa ya kulevya aina ya heroine yenye uzito wa kilo 2.188.

 

Mshitakiwa hakutakiwa kujibu  chochote  kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za dawa za kulevya isipokuwa Mahakama Kuu au hadi Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) atoe kibali kuruhusu kesi hiyo kuendelea.

 

Mshitakiwa huyo amerudishwa mahabusu kwa kuwa mashitaka hayo hayana dhamana.

 

Rayford kwa mara  ya kwanza alifikishwa mahakamani ya Kisutu  Julai 10, 2018 na kusomewa shtaka linalomkabili.