Upepo mkali kuvuma Dar, wananchi watakiwa kuchukua tahadhari

Mkurugenzi Mkuu TMA Dkt. Agnes Kijazi

Muktasari:

  • Mamlaka ya Hali ya Hewa  imetahadharisha kwamba upepo huo mkali unazidi kasi ya kilomita 40 kwa saa na kutakuwa na mawimbi makubwa yanayozidi mita mbili.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imetoa tahadhari ya upepo mkali na mawimbi makubwa katika maeneo ya ukanda wa pwani.

Taarifa ya TMA iliyotolewa leo (Jumatatu) saa 10:00 jioni imesema upepo huo unatarajiwa kuendelea hadi kesho.

Maeneo yanayotarajiwa kuathirika ni mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam, Tanga, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.

Mamlaka imesema hali hiyo inatokana na msukumo wa upepo wa kusi unaotokana na kuimarika kwa mgandamizo mkubwa wa hewa katika ukanda wa pwani ya Tanzania. TMA imetoa angalizo kwa watumiaji wa bahari na wakazi wa maeneo hayo kuchukua tahadhari na hatua stahiki.