Upinzani, Serikali jino kwa jino Venezuela

Caracas, Venezuela. Wapinzani wa Rais Nicolas Maduro wamefunga mitaa ya Jiji la Caracas wakati wa mgomo wa saa 24 uliogeuka kuwa mapambano na kusababisha idadi ya vifo kufikia 100 na mpasuko wa Serikali umeonekana katika sura ya wananchi ughaibuni.

Upinzani uliitisha mgomo wa kitaifa Alhamisi iliyopita baada ya kura ya maoni isiyo rasmi Jumapili iliyopita kusababisha mamilioni kuukataa mpango tata wa Rais Maduro kuandika upya Katiba.

Serikali ililaani kura hiyo kwamba ni haramu, badala yake imetoa wito kupiga kura Julai 30 kuchagua Bunge Maalumu kwa ajili ya kuandika upya Katiba ya mwaka 1999.

Venezuela inahaha kujinasua kutokana na uchumi kuzidi kudidimia na wakati mwingine kuzuka mapambano ya umwagaji damu barabarani baina ya vikosi vya Serikali na wapinzani hasa baada ya Serikali kutuma jeshi mitaani kudhibiti amani na utulivu.

Mzozo mkubwa ulianza Machi baada ya Mahakama ya Juu kuhamishia mamlaka ya Bunge katika mahakama ambayo ni tiifu kwa Serikali. Upinzani uliita uamuzi huo kuwa mapinduzi na baadaye mahakama ilitengua uamuzi wake.