Upinzani kuadhibu wanachama wake

Raila Odinga

Muktasari:

ODM itaandaa mikutano katika maeneo kadha ya kaunti hiyo kama njia mojawapo ya kuhamasisha wanachama wake.


BUSIA, Kenya. Chama cha Upinzani ODM katika kaunti ya Busia kimesema kitawaadhibu wanachama hasimu ambao wanavunja kanuni zake.

Katibu wa chama hicho Busia, Innocent Oluku amesema chama hicho hakitakubali wanachama ambao wanazidi kupinga mchakato wa kurekebisha katiba inavyopendekezwa na kiongozi wao Raila Odinga.

“Hili ni shughuli ambayo itaendelezwa kote nchini ili kurejesha hadhi ya chama kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2018. Vilevile tunalenga kukiimarisha chama baada ya chaguzi hizo kuzua tofauti,” amesema  Oluku.

Baadhi ya viongozi wanaolengwa ni madiwani wakiwemo wale wateule na vile vile viongozi katika matawi ya chama wilayani.

Amesema ametambua kuwa licha ya Odinga kufikia mapatano na Rais Uhuru Kenyatta, jitihada zao za kuhakikisha katiba inafanyiwa marekebisho ili kuwezesha mfumo wa rais kuchaguliwa na Bunge la kitaifa unatumika.

Katika harakati za kukipa sura mpya chama hicho maarufu hasa eneo la Magharibi na Pwani, kiongozi huyo ameongeza kuwa ODM itaandaa mikutano katika maeneo kadha ya kaunti hiyo kama njia mojawapo ya kuhamasisha wanachama wake.