Upinzani wahoji mkanganyiko akiba ya chakula nchini

Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kuhusu Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mbunge wa Viti maalumu (Chadema), Cecilia Pareso

Muktasari:

Akiwasilisha hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kuhusu Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mbunge wa Viti maalumu (Chadema), Cecilia Pareso alisema takwimu hizo zina utata.

Dodoma. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeitaka Serikali kutoa maelezo ya mkanganyiko uliojitokeza kuhusu akiba ya chakula na kupanda kwa kasi kwa bei ya mahindi nchini.

Akiwasilisha hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kuhusu Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mbunge wa Viti maalumu (Chadema), Cecilia Pareso alisema takwimu hizo zina utata.

Pareso alisema takwimu zinaonyesha mahitaji ya chakula kwa msimu wa 2016/2017 ni tani 13,159,326 na kati ya hizo, mahitaji ya nafaka yalikuwa ni tani 8,355,515 na tani 4,803,560 isiyo na nafaka.

“Kwa taarifa hiyo kunaonyesha kuwapo ziada ya chakula tani 3,013,515 na hivyo Taifa kuwa na utoshelevu wa asilimia 123 ikilinganishwa na asilimia 120 kwa mwaka 2015/16,” alisema na kuongeza;-

“Pamoja na uzalishaji wa ziada, halmashauri 55 zilikuwa na ukosefu wa chakula na jumla ya watu 1,186,028 walikuwa na mahitaji ya jumla ya tani 35,491.”

Kwa mujibu wa Pareso, kambi hiyo inaona Serikali inatakiwa kutoa maelezo kuhusu takwimu hizo za ziada ya tani 3,013,515 na hapohapo halmashauri 55 zikatajwa kuwa na upungufu wa chakula.

Pareso alisema kwa mujibu wa utafiti wa bei za mazao ya vyakula uliofanywa kwenye maeneo mbalimbali nchini, unaonyesha kupanda kwa kasi kwa bei ya unga maeneo mengi nchini.

Alisema mfuko wa sembe wa kilo 25 uliokuwa ukinunuliwa kwa Sh18,000 sasa unauzwa hadi Sh40,000 wakati Mtwara ulikuwa ukiuzwa Sh27,000 lakini sasa unauzwa Sh40,000.

Mbali na suala hilo, lakini kambi hiyo imeitaka Serikali kuhakikisha mbegu za asili hazipotei na kusababisha kupoteza urithi wa asili kutokana na ujio wa makampuni ya kimataifa ya mbegu.

Alisema programu mbalimbali zilizozinduliwa na Serikali ili kuhakikisha mkulima anapata mbegu bora na mbolea, sahihi lakini ujio wa makampuni hayo umejiingiza kwa nguvu katika soko la pembejeo.

“Mengi yameingia kwa nguvu katika soko la pembejeo yakilenga mbegu zenye fida hasa mahindi chotara na baadhi ya aina za mpunga, biashara ambayo inategemea mbegu zilizoagizwa nje,”alisema.

Pia amehoji hatua ya Serikali kupeleka tani 140,000 za nje ya nchi wakati takwimu za Serikali yenyewe zikionyesha mahitaji kwa mwaka ni 485,000 na hadi Machi ni tani 27,000 ziliingizwa nchini.

“Hapa kuna tatizo kubwa. Kama mahitaji yetu ni makubwa na hayatimizwi lakini bado tunatoa mbolea ndani na kupeleka nje. Tatizo ni aina ya mbolea inayopelekwa nje haina ubora? Alihoji Pareso.

Hali kadhalika alisema mfumo wa usambazaji mbolea hauna uhakika kuendana na mahitaji ya wakulima kulingana na misimu ya kilimo na inapofikishwa, msimu unakuwa umemalizika.