Serikali yaanza kufufua reli ya Kaskazini

Muktasari:

Ukarabati wa reli yenye urefu wa kilomita 438 ni mkakati wa Serikali wa kufufua huduma ya usafiri wa treni nchini.

Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema wameanza kufufua reli ya Kaskazini kutoka Tanga hadi Arusha ambayo itaanza kutumika Aprili,2018.
Taarifa ya wizara iliyotolewa leo Alhamisi Desemba 14,2017 imesema reli hiyo ilikufa miaka 14 iliyopita.
Profesa Mbarawa amesema hayo alipokagua ukarabati wa reli hiyo kuanzia Korogwe hadi Mombo iliyokamilika kwa kilomita 83.
Amewahakikishia wananchi kuwa uendelezaji wa reli hiyo hadi Arusha utakamilika Aprili,2018 hivyo wataruhusu huduma za usafirishaji ziendelee na hasa mazao na bidhaa.
"Niwahakikishie wananchi kuwa kazi tuliyoianza haiwezi kusimama kwa kuwa Serikali imejipanga,” amesema.
Amemtaka Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco), Masanja Kadogosa kuongeza ajira kwa vijana wa maeneo hayo.
Profesa Mbarawa amesema Serikali itaongeza vichwa vya treni kwa kununua 11 vilivyotelekezwa katika Bandari ya Dar es Salaam kwa dola 2.4 milioni za Marekani kutoka dola 3.2 milioni.
Akizungumzia ubomoaji katika maeneo ya hifadhi ya reli, amesema ataendelea kusimamia sheria.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Rahco, Kadogosa amesema ukarabati wa reli utakuwa na mchango mkubwa kiuchumi na kijamii.
Ukarabati wa reli hiyo yenye urefu wa kilomita 438 ni mkakati wa Serikali wa kufufua huduma ya usafiri wa treni nchini.