Usajili kampuni za simu DSE washusha mauzo ya hisa

Muktasari:

Mauzo hayo ambayo yaliongezeka kwa zaidi ya mara mbili mwanzoni mwa mwezi huu, yamepungua kutoka hisa milioni 2.8 zilizouzwa kwenye wiki ya kwanza mpaka hisa 500,000 na kuiingizia DSE Sh5.5 bilioni zikilinganishwa na Sh13.2 bilioni za juma lililotangulia.

Dar es Salaam. Wakati kampuni za mawasiliano zikitarajiwa kuorodheshwa, mauzo ya hisa kwenye Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) yameshuka kwa zaidi ya asilimia 80 kwa wiki iliyoishia Januari 13.

Mauzo hayo ambayo yaliongezeka kwa zaidi ya mara mbili mwanzoni mwa mwezi huu, yamepungua kutoka hisa milioni 2.8 zilizouzwa kwenye wiki ya kwanza mpaka hisa 500,000 na kuiingizia DSE Sh5.5 bilioni zikilinganishwa na Sh13.2 bilioni za juma lililotangulia.

Meneja Miradi wa DSE, Patrick Mususa alisema chanzo cha kupungua kwa mauzo ya hisa kinaashiria maandalizi ya wawekezaji kushiriki kwenye mauzo ya awali ya kampuni za mawasiliano yanayotarajiwa kufanyika muda wowote mwaka huu.

Alisema kwa kuzingatia shauku hiyo, soko hilo linaendelea kutoa elimu kwa wananchi hasa wanafunzi wa vyuo vikuu ili kuongeza ushiriki. “Mashindano ya wanafunzi wa vyuo vikuu ni mradi wa kutoa elimu wanaochukua shahada za kwanza, uzamili na uzamivu. Wanafunzi hawa watakuwa walimu wa kuelimisha wazazi, ndugu na familia zao kwa ujumla,” alisema Mususa.

Alifafanua, licha ya uwapo wa zaidi ya Watanzania milioni 39 wenye kipato halali kutokana na shughuli zao, wanaoshiriki kinachoendelea sokoni hapo hawafiki milioni moja hivyo kuna haja ya elimu ya kuongeza hamasa kwa wananchi. Mpaka sasa, kampuni tatu za Airtel, Vodacom na Tigo ambazo zinahudumia zaidi ya asilimia 80 ya wateja wote wa simu za mkononi zimewasilisha maombi ya kusajiliwa DSE. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), mpaka Juni mwaka jana, kulikuwa na watumiaji milioni 39.2 milioni.

Wakati mauzo ya hisa yakishuka, ya hati fungani yamepanda kwa theluthi moja kutoka Sh131.8 milioni mpaka Sh172 milioni ndani ya muda huo.

Taarifa ya kila wiki ya DSE inaeleza: “Hati fungani mbili za Serikali zenye thamani ya Sh76 milioni na moja ya Benki ya Exim ya Sh96 milioni ziliuzwa na kununuliwa.

Kwenye mauzo ya hisa, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) iliendelea kufanya vizuri baada ya kuuza asilimia 98.3 ya jumla ya hisa zote na kufuatiwa na Kampuni ya Sigara nchini (TCC) iliyouza asilimia 0.7 na Benki ya NMB asilimia 0.6.

Vilevile, ukubwa wa mtaji wa kampuni zilizoorodheshwa katika soko hilo umeongezeka kwa Sh500 bilioni kutoka Sh18.6 trilioni hadi Sh19.1trilioni wakati ule wa kampuni za ndani ukiendelea kubaki kwenye kiwango kilekile cha Sh7.5 trilioni.