Usalama Kibiti ulivyozua mjadala katikati ya utafiti wa Twaweza

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze akitoa ufafanuzi kwa wadau na waandishi wa habari baada ya kutangaza matokeo ya utafiti kuhusu Usalama, Polisi na Haki jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Katika utafiti huo unaoitwa ‘Hapa Usalama Tu: Usalama, Polisi na Haki nchini Tanzania’ unaonyesha kuwa asilimia 53 ya wananchi waliohojiwa walisema usalama wa nchi umeimarika wakati asilimia 37 wakisema hali imebaki vilevile huku asilimia 10 wakidai kuwa hali imekuwa mbaya zaidi.

Dar es Salaam. Wakati utafiti uliofanywa na Taasisi ya Twaweza ukionyesha kuwa hali ya usalama nchini imeimarishwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, wachambuzi mbalimbali wakiwamo wa haki za binadamu wamehoji kuhusu maeneo la Kibiti, Mkuranga na Rufiji mkoani Pwani.

Katika utafiti huo unaoitwa ‘Hapa Usalama Tu: Usalama, Polisi na Haki nchini Tanzania’ unaonyesha kuwa asilimia 53 ya wananchi waliohojiwa walisema usalama wa nchi umeimarika wakati asilimia 37 wakisema hali imebaki vilevile huku asilimia 10 wakidai kuwa hali imekuwa mbaya zaidi.

Wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga zimekuwa zikikumbwa na matukio ya mauaji dhidi ya viongozi wa vijiji tangu Mei 2016 na mengi yamekuwa yakifanyika usiku kwenye nyumba za viongozi hao na watu wengine waliowahi kushika nyadhifa za uongozi na askari.

Ripoti ya utafiti iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze inasema mtazamo wa jumla unaonyesha usalama wa nchi umeimarika katika kipindi cha mwaka uliopita.

Eliyakuze alisema sauti za wananchi hao mwaka 2015 zilionyesha kuwa asilimia 57 hawakuwahi kuhisi kuwa wako salama kutembea kwenye maeneo wanayoishi, lakini mwaka huu idadi imeongezeka hadi asilimia 71.

Alisema kuwa takwimu za utafiti huo zilikusanywa mwezi Aprili kutoka kwa watu 1,805 wa maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara ukiwa ni uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mkononi.

Maoni ya wadau

Wakichambua utafiti huo, baadhi ya wachambuzi walisema licha ya matokeo kuonyesha kwamba hali ya usalama imeimarika, lakini kwa baadhi ya maeneo hasa mkoani Pwani bado kuna hofu.

Mkurugenzi wa Jamii Forum, Maxence Melo alisema eneo la Kibiti mkoani Pwani linasababisha wananchi kuona kama hawapo salama na kwamba, iwapo utafiti huo ungejikita kuwahoji wananchi wengi wa Kibiti ungeathiri hata matokeo yake.

Melo alilishauri Jeshi la Polisi kuacha utamaduni wa kubandika namba kwenye mbao za matangazo, badala yake litumie vyombo vya habari ikiwamo mitandao ya kijamii ili wananchi wapate namba za dharura zitakazowawezesha kuripoti matukio ya uhalifu.

“Kama tukiwa wakweli hapa tulipo nani ambaye anakiri anakumbuka namba za dharura za polisi, itafutwe namna wananchi wajue wanawezaje kuripoti matukio ili kuongeza imani kwa Jeshi la Polisi zaidi ya hata sungusungu,” alisema.

Mratibu wa Taifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa alisema hali ya usalama wa watu na mali zao kwenye baadhi ya maeneo bado ni tatizo.

Olengurumwa alisema kuwa eneo la Kibiti limetikisika kiusalama japokuwa alikubaliana na matokeo ya Twaweza kwamba, kidogo kuna unafuu kwa kuwa Serikali imejaribu kupunguza hali hiyo sambamba na ile ya utendaji wa haki hasa watu wenye nguvu katika jamii wanapokutwa na makosa ya uhalifu.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHLC), Anna Hanga alisema hivi sasa watu wamekuwa waoga kutokana na matukio yanayoendelea Kibiti, Mkuranga na Rufiji.

Alisema kwa kuwa matokeo ya utafiti hupingwa na utafiti na kwamba yale yao ya awali kuhusu hali ya usalama nchini yanapingana na yaliyoripotiwa na Twaweza.

Mwanaharakati wa masuala ya Jinsia, Profesa Marjorie Mbilinyi alisema utafiti huo haukujikita kwenye masuala ya usalama kuhusu ukatili wa kijinsia wanaofanyiwa watoto na wanawake, ikiwamo ubakaji.

Profesa Mbilinyi alisema kama utafiti huo ungegusia hali hiyo, yangepatikana matokeo ambayo yangeonyesha hali halisi kuhusu ukatili unaoendelea dhidi ya makundi hayo.

“Tunasikia matukio ya watoto kufanyiwa ukatili, nadhani huu utafiti umejikita zaidi kwenye uhalifu. Nadhani pia ungeangalia hata usalama hasa kwa makundi yanayofanyiwa ukatili,” alisisitiza.

Utafiti wenyewe

Hata hivyo, akifafanua kuhusu utafiti huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Eliyakuze alisema asilimia 16 ya wananchi walikiri kukaa majumbani mwao huku wakiwa na hofu ya uhalifu.

Alisema utafiti huo haukujikita sehemu moja isipokuwa kwenye maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara. Hata hivyo haukufanyika Zanzibar.

Eliyakuze alisema pamoja na viashiria vya usalama kuwa juu, utafiti huo unaonyesha kuwa viwango vya uhalifu vimeonekana viko juu.

“Asilimia 41 ya wananchi waliwahi kushuhudia uhalifu ukifanyika hadharani ndani ya mwaka uliopita na wizi unatajwa kuwa tishio kubwa,” alisema.

Pia, alisema kati ya wananchi wanaotoa taarifa polisi kuhusu uhalifu, asilimia 26 walisema kuwa hawaridhiki na huduma wanayopewa.