Ushauri wa Mrema kwa polisi, mahakama

Mwenyekiti wa Bodi ya Msamaha kwa Wafungwa (Parole), Augustine Mrema

Muktasari:

Asema wanastahili kifungo cha nje, daktari aeleza aina za tiba zinazowafaa

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya Msamaha kwa Wafungwa (Parole), Augustine Mrema ameliomba Jeshi la Polisi na Mahakama kutowapeleka wahanga wa dawa ya kulevya jela, badala yake wapelekwe katika tiba kwa kufungwa vifungo vya nje ili kuipunguzia Serikali gharama.

Akizungumza jijini hapa jana, Mrema alisema waathirika wa dawa za kulevya wana mchango mkubwa endapo watasaidiwa na kurekebishwa na Serikali pamoja na jamii.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kuratibu Dawa za Kulevya ya Septemba, 2015 kipengele cha 31 inatoa mbadala wa adhabu hiyo ambayo inaisaidia nchi katika kuongeza kipato.

“Nimetoa ushauri badala ya kuwapeleka gerezani waathirika hao, wapelekwe hospitalini na waanzishiwe dawa ili kuwarejesha katika utu wao wa zamani,” alisema Mrema.

Mwenyekiti huyo alisema alianza kufanya mikutano na baadhi ya vijana walioathirika na dawa hizo jijini Dar es Salaam ambao wengi walidai hawana shughuli maalumu.

Alisema baadhi yao walimhakikisha kwamba wako tayari kulima kama watapewa mashamba na kufanya usafi katika maeneo ya umma kwa ujira wowote.

Katika mikutano na waathirika hao, alisema vijana hao wako tayari kushirikiana na polisi kuwafichua wauzaji wakubwa wa dawahizo hapa nchini.

Pia, alisema dawa za kulevya zinarudisha nyuma maendeleo ya nchi, kwani asilimia kubwa ya vijana ndio wamekuwa waathirika na Dar es Salaam pekee inao zaidi ya 3,000 waliotambuliwa.

Mrema aliitaka Serikali kuongeza idadi ya vituo vitakavyotoa huduma ya kuwasaidia vijana hao ambayo kwa sasa inapatikana katika hospitali za Muhimbili, Mwananyamala na Temeke .

Alisisitiza kwamba bila kufanya hivyo magereza yatajaa, huku nguvu kazi ya Taifa ikipotea.

Daktari wa Masuala ya Akili kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Kasian Nyandindi alieleza kuwa tiba ziko za aina tatu na mwathirika anaweza kuzifuata, huku ya kwanza ikiwa ni kupitia semina kwa ajili ya ili kubadilishana mawazo, dawa za Methadone na kufanya shughuli mbalimbali.

“Njia nzuri ya kuwaondoa vijana katika dawa za kulevya ni kuwapatia shughuli za kufanya zitakazowafanya kuwa kazini muda mwingi badala ya kukaa vijiweni bila kazi,” alisema Dk Nyandindi.