Ushindi wa CCM waishtua Chadema

Muktasari:

Hatua hiyo inaonyesha kuanza kurejea kwa uhai wa chama hicho ambacho kilipoteza mvuto mkoani Kilimanjaro

Moshi. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimeanza kujiimarisha baada ya kushinda uchaguzi wa mwenyekiti wa mtaa na mjumbe katika mji wa Moshi, ushindi ambao umeishtua Chadema.

Kwa miaka 20, Jimbo la Moshi Mjini limekuwa chini ya ngome ya upinzani katika nafasi ya ubunge na tangu 2010, Baraza la Madiwani wa halmashauri lipo chini ya Chadema.

Katika uchaguzi huo uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, mgombea wa CCM, Salvatory Chati alimshinda mgombea wa Chadema kwa nafasi ya uenyekiti wa Mtaa wa Vijana Kata ya Korongoni, Hatibu Kimario kwa kura 280 dhidi ya 128.

Pia, katika uchaguzi wa kujaza nafasi ya mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kiusa Laini, mgombea wa CCM, Asha Issa aliibuka kidedea kwa kura 66 dhidi ya sita za mgombea wa Chadema, Lilian Kimario.

Akizungumzia matokeo hayo, Katibu wa CCM Moshi Mjini, Loth Ole Nesele alisema wananchi wakipa chama hicho ushindi kwa sababu wanakiamini kitawaletea maendeleo ya kweli.

“Hivi sasa (wananchi) wametambua mchele na chuya ni zipi. Zile blahblah wameshazishtukia. Rais wetu mpendwa na viongozi wetu wa CCM wamerudisha imani ya wananchi kwa CCM,” alisema.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema alisema kisiasa matokeo hayo yamewaaamsha na sasa wanajua wana changamoto kuhakikisha wanashinda uchaguzi utakaojitokeza.

Alisema wanakaa kujipanga upya kuona walipojikwaa, kwani siyo kawaida kwa chama hicho kupoteza ushindi kwa urahisi.