Ushirikiano wa AQRB, wahandisi wa nje wapigiwa chapuo

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema hayo kwenye mafunzo endelevu ya 27 ya bodi  hiyo yanayofanyika jijini Mwanza.

Muktasari:

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema hayo kwenye mafunzo endelevu ya 27 ya bodi  hiyo yanayofanyika jijini Mwanza.

Mwanza.  Serikali imeitaka Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majengo nchini (AQRB) kushirikiana na wataalamu kutoka nchi jirani katika kutoa mafunzo kwa wataalamu wa ujenzi.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema hayo kwenye mafunzo endelevu ya 27 ya bodi  hiyo yanayofanyika jijini Mwanza.

Profesa Mbarawa amesema kwa kutumia wataalamu kutoka nje ya nchi, itasaidia kubadilishana uzoefu pamoja na kuendana na soko la ushindani.

Pia, amewataka wanachama wa bodi hiyom kutumia elimu waliyo nayo kwa uadilifu wakati wanapopata fursa za ujenzi katika miradi mbalimbali kwa ajili ya masilahi ya Taifa.

Naye Kaimu Msajili wa bodi hiyo, Albert Munuo amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwaelimisha wataalamu na wadau wa sekta ya ujenzi kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodi, Dk Ambwene Mwakyusa, amesema wameanza kutoa vifaa vya maabara za sayansi, vyenye thamani ya Sh3 milioni ili kuhamasisha vijana wanaosoma masomo ya sayansi.

Amesema mpango huo utakuwa endelevu na ni kwa ajili ya vijana wote wa Kitanzania wanaopenda masomo hayo.