Usiyoyajua sakata la shamba la Sumaye

Eneo la shamba la mke wa Sumaye ambalo limevunwa mahindi mwaka huu.

Muktasari:

Maswali mengi ni kuhusu sababu za kuonekana anaandamwa zaidi na Serikali katika umiliki wa ardhi kulinganisha na wanasiasa wengine.

Morogoro. Uamuzi wa Rais John Magufuli kufuta hati ya umiliki wa shamba la Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye umeibua maswali tofauti katika kipindi ambacho mwanasiasa huyo wa upinzani amefutiwa hati nyingine ya eneo lake jijini Dar es Salaam.

Maswali mengi ni kuhusu sababu za kuonekana anaandamwa zaidi na Serikali katika umiliki wa ardhi kulinganisha na wanasiasa wengine.

Maswali mengine ni kuhusu sababu za kufutwa hati ya shamba lote wakati waziri huyo mkuu wa zamani ameshaendeleza sehemu ya eneo hilo na kama atalipwa fidia.

Katika mahojiano na Mwananchi hivi karibuni, Sumaye, Waziri Mkuu pekee aliyeshika wadhifa huo kwa miaka yote kumi, alisema kuna watu wengi na tena wanajulikana ambao wanamiliki ardhi ya ukubwa wa hadi ekari 100,000, lakini hawabughudhiwi.

Kwa mtazamo wake ni kwamba anasumbuliwa kwa sababu amehamia upinzani baada ya kuihama CCM mwaka 2015 na kujiunga na Chadema.

Shamba ambalo Rais alifuta hati yake juzi ni la ekari 426 na liko Kijiji cha Mvomero mkoani Morogoro, kijiji ambacho sensa ya mwaka 2012 zinaonyesha kina watu 37,321 kati ya watu 312,109 waishio wilaya ya Mvemero na eneo la kilomita 1,133 za mraba.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Mwananchi ilizipata katika eneo hilo, shamba hilo linamilikiwa na Esther Sumaye, ambaye ni mke wa waziri huyo mkuu wa zamani.

Hoja zilizotolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kufuta hati hiyo ni kutokana na Sumaye kutoendeleza shamba hilo.

Taarifa za kufutwa kwa hati hiyo zimewachanganya watu wanaoishi eneo hilo ambao waandishi wa gazeti hili walibahatika kuwakuta juzi.

“Mimi na familia yangu ndio maisha yetu yako hapa na hatujui baada ya agizo hili la Serikali,” alisema Catherine Sumaye, mtu aliyejitambulisha kuwa ni mke wa Emmanuel Sumaye, ambaye ni mdogo wa waziri huyo mkuu wa zamani.

Katika eneo hilo kuna shamba la ekari takriban mbili lililolimwa mahindi na kuna ghala lenye magunia ya mahindi yapatayo 60 ya kilo 100 kila moja yaliyovunwa.

Eneo jingine lina banda la ng’ombe wapatao 30 na ndama takriban 15, wakati nje ya nyumba waishio wawili hao kuna trekta ambalo Catherine alisema hutumika kulimia.

Kabla ya kuzungumza na waandishi wa Mwananchi, mtoto wa kike wa mama huyo aitwaye Amina aliibuka na simu na kumpa mwenzetu mmoja azungumze nayo.

Alikuwa ni Waziri Mkuu aliyetaka kujua sababu za waandishi wa Mwananchi kufika eneo hilo, na alipoelezwa kuwa lengo lilikuwa ni kujionea uendelezaji uliofanywa katika eneo hilo, aliagiza waliokuwepo eneo hilo kutoa ushirikiano.

“Familia ina ng’ombe 1,500, lakini wengine tuliwahamisha kwa sababu ya ukame,” alisema Catherine.

Pia alisema wana mbuzi 150 na kunyoosha mkono kuonyesha eneo ambalo limelimwa mahindi na alizeti kuzunguka nyumba wanayoishi. Eneo lililolimwa halizidi ekari tatu.

Alipoulizwa kuhusu shughuli zinazofanyika katika eneo lililosalia, Catherine alisema zinatumika kwa ajili ya malisho ya mifugo inayomilikiwa na familia hiyo.

“Ukiwa mfugaji huwezi kulima eneo lote, lazima ubakize eneo kwa ajili ya malisho ya mifugo kwa kuwa kipindi cha kiangazi tunapata taabu sana ya malisho kwa mifugo yetu,” alisema mama huyo.

Alipoulizwa kama mifugo iliyohamishwa kwa ajili ya ukame itarejeshwa, alijibu kuwa walikuwa wanakusudia kuirejesha kwa kuwa hawana mahali pengine.

Tutatumia eneo kujenga shule

Mwananchi ilipomtafuta mwanyekiti wa Kijiji cha Mvomero, Victor Ngulungwa kuzungumzia suala hilo, alionekana kufurahishwa na uamuzi wa Serikali, akisema wamelifuatilia tangu mwaka 2003.

“Ukweli ni kwamba shamba hili ni pori, eneo linalotumika ni kama ekari mbili tu wakati maelfu ya wananchi wangu hawana hata maeneo ya makazi wala ya kuendeshea shughuli za kilimo,” alisema.

Alisema wanatarajia kujenga shule ya msingi katika eneo hilo kwa kuwa zilizopo hazitoshi wanafunzi kiasi cha darasa moja kuchukua hadi wanafunzi 200.

Pia, alisema eneo lililobaki katika shamba hilo lililo umbali wa mita 500 kutoka Barabara ya Magole-Turiani na takriban kilomita tisa kutoka Barabara ya Morogoro-Dodoma, watalitumia kugawa viwanja.

Hata hivyo, Ngulungwa alisema baada ya Serikali kufuta hati ya umiliki, watamgawia Sumaye sehemu ya ardhi hiyo. “Akiomba tutamfikiria pia kama tutakavyofikiria waombaji wengine,” alisema.

Ngulungwa alisema Serikali haipaswi kulaumiwa kubatilisha hati hiyo kwa kuwa shamba hilo lina vichaka ambavyo ni hatarishi na wananchi walisharipoti kuonekana kwa chatu.

“Nimepokea malalamiko mara kadhaa kuhusu kuonekana kwa chatu katika pori la shamba hili na nilishatoa taarifa polisi na maliasili, lakini bado hatujafanikiwa kumuua,” alisema.

Mgogoro wa shamba na CCM

Shamba hilo pia lina chembechembe za kisiasa, kwa mujibu wa mwenyekiti wa Kitongoji cha Kipogolo, Abdallah Madebe.

Madebe alisema kutotatuliwa kwa mgogoro wa shamba hilo kulikuwa kunahatarisha uhai wa CCM na ulisababisha wengi kukihama chama hicho.

Alisema mgogoro huo ndio chanzo cha serikali ya kijiji hicho kuongozwa na upinzani ambapo kati ya wajumbe 25 wa kijiji hicho wawili tu ndio wanaotoka CCM huku waliobaki wakitoka CUF na Chadema wakati mwenyekiti anatoka UPDP

Mkazi wa kijiji hicho, Ali Makao alisema kurejeshwa kwa shamba hilo kutarejesha nguvu ya CCM ambayo ilishatoweka kijijini hapo.

Hisia kama hizo anazo binti wa mdogo wake Sumaye anayeitwa Amina.

Amina alisema wamekuwa wakishiriki katika shughuli za kijamii kama kuchangia mwenge, madawati na shughuli nyingine, lakini kitendo cha kuhamia upinzani kimesababisha baba yake mkubwa anyang’anywe mashamba.

Lukuvi: Tumefuta hati

Akizungumzia sakata hilo, Waziri Lukuvi alisema kufuta hati si kunyang’anywa ardhi na mali nyingine na hivyo kama Sumaye alikuwa ameendeleza sehemu ya shamba atafidiwa mali zake.

Lukuvi alikuwa na angalizo katika hilo. “Kama kuna maendelezo (uwekezaji) ya kudumu, basi tathmini itafanyika na atalipwa fidia ya mali zilizomo kwenye shamba hilo.”

Alisema shamba linapochukuliwa kwa ajili ya maslahi ya umma, mmiliki hufidiwa, lakini shamba la Sumaye limefutwa hati ya umiliki hivyo hawezi kulipwa.

“Lazima mjue kuna tofauti kati ya shamba kuchukuliwa kwa maslahi ya umma na kufutwa kwa hati ya umiliki,” alisema Lukuvi.

Akizungumza kwa ufupi, Lukuvi alisema Sumaye pia alibadili matumizi ya ardhi kwa kuwa badala ya kulitumia kwa kilimo, alianza kulitumia kwa ufugaji, kitu ambacho ni kinyume na makubaliano.

Alisema tatizo la Sumaye aliendeleza sehemu ndogo ya shamba na ilikuwa vigumu kumfikiria kutokana na uwiano wa eneo lililoendelezwa na lililoachwa kuwa pori.

Lukuvi alisema hatua zote zilifuatwa kabla ya kufikia uamuzi huo kwa halmashauri kutoa notisi ya siku tisini kwa mmiliki na baadaye kupeleka mapendekezo kwa wizara ambayo huidhinisha kabla ya kumpelekea Rais kufuta hati ya umiliki.